Wazazi watakiwa kutowafisha wanafunzi wenye ulemavu Dodoma
Na. Leah Mabalwe, DODOMA MAKULU
Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri amewataka wazazi kutowaficha watoto
wenye uhitaji maalum na badala yake kuwapeleka shule kwa sababu nao wanatakiwa
kupata elimu iliyo bora.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akikagua kazi za watoto wenye mahitaji maalum
Kauli
hiyo aliitoa alipokuwa akiongea na Jumuiya ya Shule ya Msingi Dodoma Viziwi
alipofanya ziara ya kawaida kutembelea shule hiyo iliyopo katika Halmashauri ya
Jiji la Dodoma.
Alhaji
Shekimweri alisema kuwa kila mzazi anatakiwa kumpeleka mtoto wake shule hata
kama anaulemavu kwasababu ni haki yake ya msingi. “Nitoe kauli hii kwa wazazi
wote, kila mtoto asiachwe nyuma, kila mtoto ananafasi ya kupata elimu na sio
elimu tu na baadae kuweza kuitumikia nchi katika nafasi mbalimbali. Wazazi wote
wasifiche watotot wao wenye changamoto wakakosa nafasi ya kusoma, sio tu
mnakuwa hamuwatendei haki watoto bali hamjitendei haki nyie kama wazazi. Wapo wazazi
ambao wanawaficha watoto wao wenye ulemavu na kuwapendelea wasio kuwa na
changamoto hizo, msifanye hivyo, kwa sababu hakuna ajuae mpango wa Mwenyezi Mungu”
alisema Alhaji Shekimweri.
Aidha,
mkuu huyo wa wilaya aliwataka wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kuwa na nidhamu
na kufuata taratibu zilizowekwa na kuwasikiliza wanaosimamia taaluma. “Na
niendelee kuwaomba wanafunzi wote wanaosoma katika shule hii kuendelea kuwa na
nizamu, kuendelea kufuata taratibu za kuishi kwenye maeneo rasmi kama hapa,
kuendelea kuwasikiliza wanao simamia taaluma pamoja na nidhamu na wanafanya
haya yote kwa manufaa yenu ninyi wenyewe, manufaa ya nchi yetu na manufaa ya
wazazi wenu. Nawaomba muwe na nidhamu na msome kwa bidii na kila mmoja aweke
malengo makubwa na mwisho wasiku kuyafikia malengo yake’’ alisema Alhaji Shekimweri.
Mkuu
wa wilaya aliwashukuru walimu wote wa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi kwa kuwa na
moyo wa kujitoa kwaajili ya watoto wenye uhitaji maalumu. “Nawashukuru sana
walimu wote mnaofundisha katika shule hii, tunawashukuru sana kwa kazi kubwa na
nzuri mnayoifanya. Mimi naamini kukaa na watoto wa namna hii inabidi uwe na
moyo wa upendo na kujitoa sana, mnafanya kazi nzuri sana na nazidi kuwaombea
muwe na moyo huohuo wa upendo kwa watoto na Mwenyezi Mungu atawabariki sana” alisisitiza
Alhaji Shekimweri.
Awali
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi, Mwl. Awadhi Mbogo akiwasilisha
taarifa ya shule ya shule hiyo kwa mkuu wa wilaya alisema kuwa shule hiyo
ilipanga kuandikisha wanafunzi 12 wa elimu awali na wanafunzi 24 wa darasa la
kwanza. “Mpaka sasa tumeandikisha wavulana saba na wasichana sita jumla 13 kwa darasa
la kwanza na darasa la awali wavulana watano na wasichana wanne jumla tisa.
Hivyo, kufanya jumla ya walioandikishwa mwaka 2024 kuwa 22 kati ya 34 ya lengo sawa
na asilimia 61. Tunaendelea kutoa elimu katika jamii kwa kutembelea shule na
mitaa mbalimbali ili kuhakikisha tunafikia lengo la uandikishaji kwa asilimia
100” alisema Mwl. Mbogo.
Shule
ya Msingi Dodoma Viziwi ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na jumla ya wanafunzi
watano lengo likiwa ni kutoa fursa ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum (viziwi).
MWISHO
Comments
Post a Comment