DC Shekimweri awataka wazazi kuwa karibu na watoto wao

Na. Arafa Waziri, DODOMA MAKULU

Mkuu wa Wilaya wa Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kuwaepusha  na vitendo vya kikatili ili wawe katika mazingira salama.

 

Mkuu wa Wilaya wa Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri akiongea na walimu na wazazi 


Aliyasema hayo wakati alipotembelea Shule ya Msingi Kisasa na kuongea na walimu na wazazi shuleni juu ya masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia na uelimu kwa ujumla.

Alhaj Shekimweri alisema kuwa ukatili wa kijinsia hutokea katika familia kutokana na kuaminiana sana baina ya wanafamilia. “Upo ukatili wa kijinsia, tafiti zinaonesha ukatili wa kijinsia kwa watoto asilimia kubwa wanafanyiwa na ndugu wa karibu Dunia imebadilika sana hivyo, nawasisitiza hatuna budi kuchukua tahadhari katika kuwaangalia watoto kwa karibu’’ alisema Shekimweri.

Alisema kuwa ni vema wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao kwa kuangalia watu wanaokutana na kuhusiana nao ili kubaini kama wanafaa kumjenga mtoto huyo kitaaluma. “Kijana wako ana marafiki gani anaokutana nao, wanaokuja nyumbani anamsaidia ama anampotosha mtoto wako?. Kwahiyo, niwaombe kama mzazi kuangalia marafiki wenye mchango wa watoto katika taaluma ya mtoto” alisema Alhaj Shekimweri.

Vilevile, alisisitiza wazazi kusimamia maadili ya watoto na kuepuka kuwapa adhabu kali ambazo zinasababisha kuathirika kisaikolojia. “Ukatili mwingine una athiri katika maendeleo ya mtoto kielimu, ni wajibu kama wazazi kusimamia maadili na kuwapa adhabu za kumfanya mtoto kujua amekosea na sio adhabu za kumuumiza mtoto kiasi cha kutoelwa darasani” alisema Shekimweri.

Kwa upande mwingine, aliwataka walimu kumaliza silabasi kwa wakati ili wanafunzi wapate muda mzuri wa kujisomea. Kumaliza silabasi mapema pia kunawapa nafasi wanafunzi kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mitihani. “Walimu kukamilisha silabasi mapema ili watoto wafanye mazoezi mapema na kufaulu kwa watoto ni matokea ya watoto kufanya mazoezi na kuzoea mitihani. Hivyo, ni bora walimu kumaliza silabasi mapema ili kuwe na muda mrefu wa wanafunzi kujisomea’’ alisisitiza Shekimweri.

Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisasa, Mwl. Jesca Mwarabu wakati akisoma taarifa ya shule yake alisema kuwa imeendelea kufanya vizuri kwa upande wa taaluma kwa mitihani ya ndani pamoja na mitihani ya kitaifa.  Kwa miaka mitatu mfululizo shule imekuwa ikifaulisha kwa asilimia 99.

Walimu, wazazi pamoja na walezi wanamchango mkubwa katika kumkuza mtoto katika maadili na taaluma bora hivyo ni wajibu wao kushirikiana na hatimae kuwa na jamii bora.

 

MWISHO

 

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma