Jiji la Dodoma lasafisha korongo la Kishoka kuondoa kero ya mafuriko kwa wananchi
Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma
imesikia kilio cha wakazi wa Mtaa wa Kishoka, Kata ya Chang’ombe cha kero ya
kuziba kwa korongo linalopitisha maji ya mvua na kusababisha mafuriko katika
makazi yao.
![]() |
Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga akiongelea zoezi la kuondoa taka katika korongo la Mtaa wa Kishoka |
Katika utatuzi wa kero hiyo Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imepeleka mtambo (JCB Backhoer) kwa ajili ya kufukua korongo
hilo na kuondoa taka ngumu zilizotupwa kwenye korongo na kusababisha maji ya
mvua kushindwa kupita.
Akiongea wakati wa utekelezaji wa
zoezi hilo Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga
alisema kuwa lengo la zoezi la kusafisha korongo hilo ni kuyawezesha maji ya
mvua yaweze kupita vizuri na kutosababisha mafuriko katika makazi ya watu. “Kama
mnavyoona hapa tunaendelea na shughuli ya siku tatu ya usafishaji wa korongo la
maji ya mvua katika Mtaa wa Kishoka, Kata ya Chang’ombe. Lengo kubwa ni
kuhakikisha tunatoa mchanga, tope pamoja na taka ngumu zote ili kutoa urahisi
wa maji ya mvua kupita vizuri kwenye korongo hili na kuzuia mafuriko katika
makazi ya wananchi. Wananchi wa eneo hili walitoa malalamiko kwa Mkurugenzi wa
Jiji la Dodoma kuhusiana na kero wanayoipata wakati wa mvua. Walisema kuwa kina
cha korongo kimepungua na hivyo, kufanya maji kutuhama kwa muda mrefu na
kusababisha yasambae kwenye makazi yao” alisema Mfinanga.
Mfinanga aliwataka wakazi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kuacha tabia ta kutupa taka ngumu katika makorongo ili
kuyaruhusu maji ya mvua kupita kwa urahisi. “Wito kwa wakazi wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, wakati halmashauri inachukua hatua ya kusafisha eneo hili kwa kuondoa
mchanga, tope na taka ngumu wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hususani
wa Mtaa wa Kishoka hakikisheni hamtumii makorongo kama sehemu ya kutupia taka
ngumu. Leo hii wote ni mashuhuda tunaona hapa korongo limeziba kwa sababu
tunatupa taka ngumu. Halmashauri imeweka utaratibu wa makampuni na vikundi kwa
ajili ya kubeba taka ngumu. Shime kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha makampuni
na vikundi vinatumiwa ipasavyo” alisema Mfinanga.
Kwa upande wake Mkazi wa Kisima cha
Nyoka Mtaa wa Kishoka, Vanesa Robert alisema kuwa kero kubwa wanayoipata wakati
wa mvua ni maji huingia katika makazi yao. “Shida tunayoipata mvua ikinyesha
yaani maji yanajaa ndani tunakosa pa kulala. Watoto wanaoenda shule wanashindwa
kwenda kwa sababu njia zinakosekana. Tunaomba mtuwekee daraja kubwa na kina cha
korongo mkirefushe ili maji yawe yanapita kwenda siyo kutuama na kuingia kwenye
makazi yetu. Kufukua mchanga huu ni usaidizi mkubwa kwetu maana mvua ikianza
kunyesha maji yatapita vizuri” alisema Robert.
![]() |
Mkazi wa Kisima cha Nyoka Mtaa wa Kishoka, Vanesa Robert akiongea kwa hisia juu ya changamoto ya maji kuingia katika makazi ya watu |
MWISHO
Comments
Post a Comment