Jiji la Dodoma kuendelea kusafisha makorongo ya maji ya mvua kuzuia mafuriko katika makazi ya wananchi
Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma itaendelea kuyafanyia usafi kwa kuondoa taka ngumu makorongo
yote ili yaweze kupitisha maji vizuri na kuondoa kero ya mafuriko wakati mvua
zinaponyesha.
![]() |
Mkuu wa Kitengo cha usafi na uthibiti wa kata ngumu, Dickson Kimaro akielezea ukubwa wa kazi ya kusafisha kongoro na kuondoa taka ngumu katika Mtaa wa Kishoka |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha usafi na uthibiti wa kata ngumu, Dickson
Kimaro alipokuwa akiongelea mipango ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika
kuhakikisha wananchi hawaathiriki na mafuriko yatokanayo ma maji ya mvua
kushindwa kupita kwenye makorongo.
Kimaro
alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaendelea kuyafanyia kazi kwa lengo la
kuhakikisha wananchi hawapati kero kama hizi zinazoonekana. Kama mnavyoona kule
mbele kuna eneo ambalo maji yakifika darajani yanagota na kurudi kuingia katika
makazi ya watu. Hapa Mtaa wa Kishoka tunasafisha korongo hili kwa kuondoa taka
ngumu na kuliongezea kina ili maji yaweze kupita vizuri ndiyo sababu mnaona
mtambo (JCB Backhoer) ukifanya kazi yake. Tukitoka hapa tutaenda maeneo mengine
mfano Kata ya Ipagala na Kizota ili kuhakikisha usalama wa wananchi unazingatiwa
katika maeneo yao kipindi mvua zinaponyesha”.
Alisema
kuwa kazi hiyo ilitanguliwa na kusafisha mitaro ya maji ya mvua katika
halmashauri na mitaro ya katikati ya mji na barabara kuu zinazoingia na kutoka
katika Jiji la Dodoma. “Kazi hii tulianza tukishirikiana na wenzetu wa Tanroads
na Tarura. Lakini kuna haya makorongo makubwa ambayo mchanga umejaa na taka
ngumu. Tutayapitia yote na kuhakikisha yanakuwa safi na kupitisha maji ya mvua
vizuri” alisema Kimaro.
Kwa
upande wake Afisa Mazingira katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga
aliwataka wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuacha tabia ta kutupa taka
ngumu katika makorongo ili kuyaruhusu maji ya mvua kupita kwa urahisi. “Wito kwa
wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wakati halmashauri inachukua hatua ya
kusafisha eneo hili kwa kuondoa mchanga, tope na taka ngumu wananchi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma hususani wa Mtaa wa Kishoka hakikisheni hamtumii makorongo
kama sehemu ya kutupia taka ngumu. Leo hii wote ni mashuhuda tunaona hapa korongo
limeziba kwa sababu tunatupa taka ngumu. Halmashauri imeweka utaratibu wa makampuni
na vikundi kwa ajili ya kubeba taka ngumu. Shime kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha
makampuni na vikundi vinatumiwa ipasavyo” alisema Mfinanga.
Nae
mkazi wa Kisima cha Nyoka, Mtaa wa Kishoka, Zawadi Juma alisema kuwa mvua
zikinyesha wanahangaika sana. “Huku wakati wa mvua tunahangaika sana. Hata
ukitaka kwenda kwenye genge huwezi kupita lazina uzunguke, hatuwezi kwenda
kununua vitu dukani kwa sababu maduka yapo upande wa pili. Watoto wanaoenda
shule au kutoka shule hawawezi sababu maji yanakuwa yamejaa hapa. Mvua inaweza
kuanza kunyesha saa 1 asubuhi hadi ikikata saa 4 kuvuka hamuwezi mpaka kesho
yake saa 1 ndio maji yanakuwa yamepungua. Kiukweli nawashukluru sana kwa sababu
serikali imeleta hii mitambo kutengeneza njia ya maji” alisema Juma.
![]() |
Mkazi wa Kisima cha Nyoka, Mtaa wa Kishoka, Zawadi Juma akiongelea changamoto ya maji kujaa katika korongo |
MWISHO
Comments
Post a Comment