ELIMU JUMUISHI KUTOA FURSA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM KUSOMA JIJI LA DODOMA
Na.
Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kujali elimu jumuishi katika
shule za awali na msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kutoa fursa
kwa watoto wengi kusoma.
Pongezi
hizo zilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipoongoza zoezi la kutoa kadi za bima za afya
na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Mlezi
iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl.
Myalla alisema “siku ya leo ni siku jumuishi ya kuhimiza elimu jumuishi kwenye
shule zetu. Tunamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kulisimamia
hilo kwenye shule zetu kama ambavyo leo tumekusanyika hapa kugawa vifaa kwa
wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum kwa shule nane zilizopo katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma. Tunaona kabisa ana nia ya dhati kuhakikisha na watoto wetu
wenye mahitaji maalum wanapata elimu iliyo sawa na watoto ambao hawana mahitaji
maalum”.
Alisema
kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa kadi za bima za afya 49
kati ya 100 kwa ajili ya kupata huduma za kiafya kwa wanafunzi wenye mahitaji
maalum. “Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeandaa vifaa vya
kufundishia na kujifunzia ili nao wapate elimu iliyo bora kwa watoto wetu wenye
mahitaji maalum kupitia shule zetu zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. Tunawashukuru wadau kwa kutoa vitimwendo kwa wanafunzi wetu wenye
ulemavu. Tunatarajia wadau wa namna hii kuendelea kuiunga mkono halmashauri
yetu. Huu ndiyo ushirikiano wa taasisi binafisi na serikali katika kuunga mkono
maendeleo ya nchi yetu kupitia elimu” aliongeza Mwl. Myalla.
Akisoma
taarifa fupi ya elimu maalum, Mkuu wa seksheni ya Elimu Maalum, Mwl. Issa Kambi
alisema “tunaishukuru serikali ya awamu ya sita, kupitia Ofisi ya Rais,
Tamisemi kwa kutenga kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 jumla ya shilingi 323,366,172
kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wenye mahitaji maalum. Kila mwezi tunapokea
jumla ya shilingi 26,947,181 kupitia ruzuku zinazoingizwa katika shule zenye
wanafunzi wenye mahitaji maalum”.
Alisema
kuwa katika bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia fedha za uendeshaji
imetenga jumla ya shilingi 26,460,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali na
ununuzi wa vifaa visaidizi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi
wenye mahitaji maalum.
Akiongea
kwa niaba ya maafisa elimu kata wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Elimu Kata
ya Hazina, Mwl. Zaituni Mkoyi alisema “kwa niaba ya maafisa elimu kata wa shule
hizi nane ambazo tumekutana hapa, naishukuru serikali na wizara zake kuona
umuhimu na kuwajali watoto hawa ambao ni kundi maalum. Nipongeze wazazi kuendelea kuwaleta watoto
ili waweze kupata elimu ambayo ni haki yao. Niombe muwe chachu na ushawishi kwa
wazazi wengine ambao bado wanaendelea kuwaficha watoto kama hawa”.
Mzazi
wa mwanafunzi mwenye mahitaji maalum, Hincha Kweji alisema kuwa walimu
wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalum wanaupendo mkubwa. “Walimu hawa
wamekuwa ni elimu kubwa sana kiasi kwamba wazazi tumefika mahali tukawapenda
watoto wetu, ina maana walimu wametufundisha kuwapenda watoto wetu wenye
mahitaji maalum” alisema Kweji.
Ikumbukwe
kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoam ina jumla ya shule 61 zinazopokea watoto
wenye mahitaji maalum, kati ya shule hizo 10 ni vitengo vya watoto wenye
mahitaji maalum na moja ni maalum na shule 50 ni jumuishi. Jiji likiwa na
wanafunzi 1,056 wenye mahitaji maalum.
MWISHO
Comments
Post a Comment