TANZANIA NA KOREA KUSINI KUSHIRIKIANA UTAFITI WA KILIMO NA TEKNOLOJIA YA KISASA YA KILIMO
Nchi za Tanzania na Korea Kusini zimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha utafiti wa kilimo na matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima wa Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Mjini Jeonju-si, Korea Kusini wakati wa mazungumzo ya
ushirikiano baina ya Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Mh. Anthony Mavunde na
Ndg. Yun Jongchul Makamu Mtawala Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Kilimo na
Utafiti ya Korea (Korea Patnership for Innovation in Agriculture- KOPIA).
Kupitia mazungumzo hayo Naibu Waziri Mavunde ameiomba KOPIA kuanzisha kituo
chake nchini Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Tanzania(TARI) ili kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi katika tafiti za
kilimo kwa lengo la kumsaidia mkulima kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa
mazao ya kilimo kwa kutumia kanuni bora za kilimo,uzalishaji mbegu bora na
teknolojia ya kisasa ya kilimo,sambamba na hayo Naibu Waziri Mavunde ameomba
pia ushirikiano wa kitaalamu katika utekelezaji wa Programu ya Vijana ya
Building a Better Tomorrow-BBT.
Naye Ndg. Yun Jongchu, Makamu Mtawala Mkuu wa KOPIA ameipongeza serikali ya
Tanzania chini ya Uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na
utashi wa kukuza sekta ya kilimo na kuongeza bajeti ya kilimo kwa kiwango
kikubwa,na kuahidi kwamba Korea Kusini kupitia KOPIA wapo tayari kushirikiana
na serikali ya Tanzania katika uanzishwaji wa kituo cha KOPIA TANZANIA ili
kusaidia katika kukuza utafiti wa kilimo na matumizi ya teknolojia ya kisasa ya
kilimo hasa katika Programu ya BBT.
Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini,Balozi Togolan Mavura ameishukuru
Taasisi ya KOPIA kwa utayari wao kufanya kazi na Tanzania na kuahidi kusimamia
makubaliano hayo ya uanzishwaji wa kituo cha KOPIA TANZANIA ambacho kitakuwa na
manufaa makubwa kwa maendeleo ya kilimo nchini Tanzania katika kutekeleza
Ajenda 10/30.
Comments
Post a Comment