WANANCHI KATA YA CHAMWINO WASHIRIKI USAFI WA PAMOJA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI
wa Kata ya Chamwino wajitokeza kushiriki usafi wa Mazingira wa kila Jumamosi
kwa lengo la kuweka Mazingira safi yanayowazunguka na kujiepusha magonjwa
yanayosababishwa na uchafu wa Mazingira.
Akiongelea
lengo la wananchi wa kata hiyo kufanya usafi wa pamoja wa Mazingira, Afisa
Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alisema kuwa ni kuhakikisha Mazingira
ya kata hiyo yanakuwa safi. “Kata ya Chamwino, usafi ni tabia yetu. Muitikio wa
wananchi kujitokeza kushiriki katika usafi wa pamoja ni mkubwa unaolenga kuweka
Mazingira safi. Muitikio huo pia ni utekelezaji wa maagizo ya viongozi wetu
kuelekeza tufanye usafi wa Mazingira ili kujihakikishia Mazingira safi na kuepuka
magonjwa yanayotokana na uchafu wa Mazingira” alisema Nkelege.
Alisema
kuwa usafi ulifanyika katika maeneo mbalimbali ukijumuisha usafi wa mitaro ya
maji ya mvua, maeneo ya biashara na maeneo ya makazi. “Maeneo haya ni muhimu
kwa sababu yanatumiwa na wananchi wengi kupata huduma” aliongeza.
Akiongelea
mitaa iliyoshiriki zoezi la usafi katika kata hiyo aliitaja kuwa ni Mtaa wa
Mwaja, Mailimbili, Sokoine na Nduka, . “Mtaa wa Mwaja usafi wa pamoja ulifanyika
katika Shule ya Msingi Chinangali ukihusisha kuzibua na kuondoa mchanga
uliofunika mitaro. Pia zoezi la kufyeka vichaka vinavyozunguka eleo la shule
ili kuwahakikishia wananfunzi na walimu Mazingira safi na salama. Kwa Mtaa wa Mailimbili, usafi
wa pamoja ulifanyika katika korongo ukihusisha kutoa taka ngumu kama makopo,
mifuko ya plastiki na kufyeka vichaka na nyasi zilizoota ndani ya korongo”
alisema Nkelege.
Mitaa mingine iliyofanya usafi wa pamoja ni Sokoine na Nduka. “Mtaa
wa Sokoine, usafi ulifanyika katika mtaro wa barabara ya Sokoine kuelekea Hoteli
ya Okaone ukihusisha kutoa taka ngumu kama makopo na mifuko ya plastiki
iliyozagaa ndani ya mtaro. Mtaa wa Nduka usafi wa jumla ulifanyika katika eneo
la wazi maarufu kwa Kimbinyiko ukihusisha kufyeka vichaka na nyasi katika eneo
hilo” alisema Nkelege.
Viongozi walioshiriki zoezi la usafi wa pamoja ni Afisa Mtendaji
Kata, Maafisa Watendaji wa Mitaa na Mwenyeviti wa Mitaa.
MWISHO
Comments
Post a Comment