JIJI LA DODOMA KUPELEKA TIMU YA MAAFISA MAZINGIRA NA AFYA KUKAGUA USAFI KATA YA IPAGALA
Na. Dennis Gondwe, IPAGALA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupeleka timu ya maafisa
mazingira na afya kufanya ukaguzi katika maeneo ya Mtaa wa Ipagala kukagua hali
ya usafi wa mazingira kutokana na changamoto wa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo
kutojitokeza kufanya usafi wa mazingira.
![]() |
Mkuu wa Kitengo cha Usafi na uthibiti taka ngumu Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro akiongea na mamia ya wakazi wa Ipagala |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na uthibiti wa taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Kata ya Ipagala waliojitokeza katika usafi wa pamoja kwenye korongo la kitaa cheusi.
Kimaro alisema “kwa sababu eneo hili lina changamoto
ya wananchi kutojitokeza kufanya usafi katika maeneo yao. Wananchi wanalalamika
kuwa watu wanaokaa kwenye nyumba zenye mageti hawajitokezi kufanya usafi na
kuwaanchia wanaoishi katika nyumba zisizo na mageti kufanya usafi. Nimetoa
maelekezo kwamba wiki ijayo kuanzia siku ya Jumatatu timu ya maafisa afya na
mazingira watapita nyumba kwa nyumba kuhamasisha usafi na ambao watakaidi
tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria”.
Akiongelea zoezi la usafi wa pamoja, alisema kuwa usafi
wa pamoja ulifanyika katika Kata ya Ipagala na Kizota. “Kwa wiki hizi mbili
tumeweka nguvu zaidi na kushiriki sisi wenyewe viongozi kwa Kata ya Ipagala na Kizota
ambapo tulibaini kuna baadhi ya maeneo ambayo ni machafu na wananchi
hawajitokezi kufanya usafi. Leo tumekuwa katika eneo la Sulungai na Ipagala
katika Korongo la Kitaa cheusi. Tumegundua wananchi wanatupa taka ovyo na
tumekuta wananchi wanatupa hata pampasi” alisema Kimaro.
Alisema kuwa kuna wakati vikundi vya kijamii ambavyo
vimepewa jukumu la kukusanya taka nao wanazitupa katika kongongo hilo. “Tumehamasisha
wananchi na kujitokeza kufanya usafi katika korongo hili na wiki iliyopita tulifanya
usafi eneo hilo. Tumetoa maelekezo kwa wananchi wote kujiepusha na tabia ya
kutupa taka ovyo kwasababu usafi ni ustaarabu na unaanza na sisi wenyewe”
alisema Kimaro.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ipagala, Elenei Mogwa
aliwashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi la usafi wa mazingira. “Zoezi
la usafi wa mazingira katika korongo hili ni zoezi endelevu mpaka korongo letu
litakapokuwa safi. Mnapowaona viongozi wa halmashauri tupo nao hapa njue ni
viongozi waliokuja kukagua usafi na kusimamia sheria. Hatua zikianza
kuchukuliwa kwa wale ambao hawatekelezi maelekezo ya usafi wa mazingira mjue ni
utekelezaji wa maelekezo rasmi kwa mujibu wa sheria” alisema Mogwa.
![]() |
Wakazi wa Ipagala wakisafisha Korongo la Kitaa Cheusi |
MWISHO
Comments
Post a Comment