AFISA MTENDAJI KATA YA CHAMWINO APEWA CHETI UTEKELEZAJI MKATABA WA LISHE JIJI LA DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
AFISA Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege amepongezwa
na kupatiwa cheti kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika
jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akimkabidhi cheti kutambua kazi nzuri ya utekelezaji Mkataba wa Lishe Afisa Mtendaji Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege |
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipoongoza Kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa robo ya nne kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Shekimweri ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alisema
kuwa suala la lishe ni muhimu kwa wilaya yake na maafisa watendaji wa kata wana
wajibu wa kusimamia lishe katika maeneo yao. “Ndugu zangu, napenda kuwaambia tunatakiwa
kuwa na tafsiri pana na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na suala la lishe. Tuhakikishe watoto wanapata
chakula shuleni. Wale wote ambao hatujafanya vizuri kwenye “score card” katika kipengele
cha chakula shuleni, niwaombe mkafanye tathmini ya kina na kuweka mikakati mahususi
na nipate taarifa ya utekelezaji wa mikakati hiyo. Aidha, mikakati hiyo iwasilishwe
kwa waratibu wa lishe. Waratibu wa lishe muandae timu ya kufuatilia ‘site’
kuangalia mikakati inavyotekelezwa. Nipo tayari na nitakuja kwenye maeneo
ambayo watu wapo tayari na wamejitoa, nije kuwaongezea nguvu. Siyo nguvu ya
maneno tu bali ya vitendo na uwezeshaji ili chakula kipatikane shuleni”.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma akisisitiza umuhimu wa Lishe kwa jamii |
Akiongelea umuhimu wa cheti cha pongezi, Afisa Mtendaji
wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alisema kuwa amehamasika zaidi kutekeleza Mkataba
wa Lishe katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Cheti hiki ambacho kinatambua
mchango wangu kufanya vizuri katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kimenipa
motisha. Nimepata motisha zaidi ya kutekeleza majukumu ya lishe. Mfano kufanya
maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe kwa mitaa na jamii kwa ujumla. Aidha, nimepata
hamasa ya kuendelea kuhamasisha lishe katika shule ili kuhakikisha wanafunzi
wanapata chakula na kutoa elimu ya lishe katika ngazi ya mtaa ili kutokomeza
hali ya udumavu na utapiamlo kwa watoto” alisema Nkelege.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Semeni Juma alisema kuwa kikao hicho kinafanya tathmini ya robo ya nne
na nusu mwaka ya mkataba wa Lishe. “Kwa kuwa tumemaliza mwaka wa fedha
2022/2023, tunafanya tathmini ya mwaka mzima kuona kiutekelezaji mkataba huu wa
lishe tumeutekeleza kwa kiasi gani ili kujipanga vizuri zaidi kwa utekelezaji
mwaka ulioanza” alisema Juma.
MWISHO
Comments
Post a Comment