Soko la Sabasaba kuongozwa kwa misingi ya uongozi bora
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Kaimu
Mkuu Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Abdul Chacha amewaasa viongozi wa Soko la Sabasaba kuzingatia weledi katika kufanya
kazi zao ili kuiishi dhana ya uongozi bora.
Aliyasema hayo katika mafunzo waliyoandaa kwa viongozi wa Soko la Sabasaba yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo kikuu cha Mabasi Dodoma.
Alisema
kuwa sifa mojawapo kubwa ya kiongozi bora ni yule mwenye kuzingatia katiba au
muongozo wa ushirika ili aweze kutenda haki. “Kiongozi bora ni yule anayejua
namna ya kutuimia katiba vizuri. Labda niulize hapa, Katiba ya ushirika ipo?
Kama ipo, je ilitumika wakati ule matatizo yameanza kutokea? Jibu litakua
hapana. Nipende kuwaambia kuwa, ukiijua vizuri katiba na miongozo, ni rahisi
sana Kutenda haki kwasababu utatenda haki kwa kuzingatia taratibu na hakuna
atakayelalamika kuwa ameonewa” alisema Chacha.
Aliongeza
kuwa zipo sifa zaidi ya 25 za kiongozi bora ambapo kila kiongozi wa soko la
sabasaba anapaswa kuzifahamu na kujijengea uwezo ili kufanya kazi kwa weledi.
“Leo tutajadiliana hizi sifa za kiongozi bora kwa pamoja. Ni muhimu kuzifahamu
ili kujiboresha hata katika utendaji wenu. Jitafakari sana kama huwezi kuwa
mbunifu au mtatuzi wa changamoto jua kuwa kuwaongoza watu itakua tatizo kwako.
Ndiyo maana leo tupo hapa kukumbushana namna kiongozi bora anapaswa kuwa
hususan kwa watu waliowachagua” aliongeza Chacha.
Nae, Mratibu wa Dawati la Wajasiriamali Mkoa wa Dodoma, Veronica Tarimo alisema kuwa mafunzo yaliyowakutanisha viongozi wa Soko la Sabasaba yatakua chachu ya mabadiliko kwa uongozi huo mpya ambao una miezi mitatu tangu kuchaguliwa kwao. “Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya ya kuwajengea uwezo namna ya kuongoza masoko na namna ya kuratibu masoko utawasidia. Tumewapatia pia elimu ya kulipa kodi kupitia mfumo wa tausi. Yote haya yataleta tija na bila shaka uongozi huu utafanya vizuri na kuwa wa tofauti” alisema Tarimo.
Kwa upande mwingine Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jumanne Sinoni alichagiza kwa kutoa elimu ya upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na kuwaalika viongozi hao kuelimisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa. “Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ina tija sana katika kukuza biashara, tuna mikopo ya makundi matatu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Ninyi viongozi mliopo hapa mkahamasishe akina mama, vijana wenu na watu wenye ulemavu wajiunge kwenye vikundi ili waje halmashauri wapate mikopo itakayo wakwamua kiuchumi” alisema Sinoni.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Kituo kikuu cha Mabasi Dodoma yakiratibiwa na Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Halmashauri ya Jiji ya Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi wa Soko la Sabasaba kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sifa za uongozi bora.
Comments
Post a Comment