Shilingi Milioni 473 kutekeleza Mradi wa Ufungaji CCTV Kamera Jiji la Dodoma
Na. Josephina Kayugwa, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imesani mkataba na Kampuni ya Wisjane Smart Systems kwaajili ya
ufungaji wa kamera za usalama barabarani (CCTV) unaogharimu shilingi 473,000,000
ikiwa ni mradi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu.
Akitoa
taarifa ya mradi, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alisema kuwa mradi huo utakwenda
kuimarisha ulinzi na usalama katika Jiji la Dodoma kwasababu kamera hizo
zitafanya kazi masaa 24. “Mradi huu wa gharama ya shilingi 473,000,000 utahusisha
ufungaji wa kamera kwenye barabara zinazoinga njia kuu lakini pia hapo baadae
utakuja kuimarishwa zaidi kwa kuongeza sehemu nyingine za kuweka kamera lengo
ni kupata picha zote za vyombo vya usafiri vitakavyokuwa vikiingia na kutoka
katika Jiji la Dodoma” alisema Fungo.
Aliongeza
kuwa wana mpango wa kuunganisha mfumo huo na taasisi nyingine ili kuimarisha
ulinzi na usalama. “Mfumo huu baada ya muda tutauunganisha na taasisi nyingine muhimu
kama vile Uhamiaji na NIDA ili kuweza kuwa na muunganiko mmoja wa kufanya kazi,
pia kuhakikisha Jiji lote linakuwa salama” aliongeza Fungo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Wisjane Smart Sytem, Wisley Ussiri ambae ni mtekelezaji wa mradi huo alisema kuwa mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu na kamera hizo zitafungwa katika barabara kuu nne za Jiji la Dodoma na zile zinazounganisha barabara kubwa. “Tunashukuru kwa kupata tenda hii ya kufunga kamera katika Jiji la Dodoma, naamini tutafanya kazi vile mkataba unavyotaka na kwa muda sahihi uliopangwa. Kwasababu tunafahamu lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi na wawekezaji wanaokuja kuwekeza jijini wanakua na uhakika wa usalama wao na mali zao” alisema Ussiri.
Comments
Post a Comment