Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ahimiza matumizi ya mfumo NeST

Na. Nancy Kivuyo, DODOMA

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko aeleza kuwa mfumo wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma NeST katika kufanya manunuzi ya vifaa vya serikali ni mfumo rafiki unaorahisisha manunuzi na kuweka taarifa hizo katika hali ya usalama.




Aliyazungumza hayo katika Baraza la Madiwani la kawaida liliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa madiwani.

Alisema kuwa mfumo wa manunuzi wa NeST upo tayari kwa mujibu wa sheria na umeonyesha matokeo chanya. “Niwajulishe ndugu wajumbe ya kwamba, mfumo huu hatuna namna ya kuepuka kuutumia kwasababu ndio mfumo ambao tunapaswa kuwa nao ili kufanikisha manunuzi ya vifaa mbalimbali vya serikali” alisema Dkt. Sagamiko.

Aliongeza kuwa mfumo haumlazimishi mnunuzi kununua kila kitu kwa wakati mmoja. “Mfumo huu unahitaji ushirikiano ili uweze kufanya manunuzi yako. Kikubwa ni wewe kuhakikisha unafahamu unafanya manunuzi ya kiwango gani. Hakikisha unafahamu mradi utekelezwa kwa ukubwa upi ili iwe rahisi kununua vifaa kwa wakati. Wengi wenu mnaogopa kufanya manunuzi kwa awamu kwa kuhofia gharama za manunuzi kuwa juu. Niwatoe hofu, mfumo ni rafiki unaweza hata kununua kifaa kimoja kwa wakati mmoja” aliongeza Dkt. Sagamiko.




Alimalizia kwa kusema kuwa watumiaji wa mfumo wa manunuzi wa NeST wawe na desturi ya kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo wakati wa matumizi ya mfumo ili kuweka mazingira mazuri ya uboreshaji wa mfumo huo. “Rai yangu ni kwamba, tutoe taarifa za changamoto ili ziwasilishwe na zifanyiwe kazi kwa maboresho zaidi. Tukifanya hivi mfumo huu utaimarika na kuendelea kutoa huduma nzuri za manunuzi na kuhakikisha kuwa kuna usiri wa nyaraka za manunuzi tofauti na kipindi cha nyuma taasisi zilikuwa zikinunua mifumo ambayo kiusalama haikuwa sawa. Waliotengeza mfumo huu ni vijana wa kitanzania hivyo tutumie vya kwetu” alimalizia Dkt. Sagamiko.




Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa rai yake ni kwamba watu wafuate utaratibu wa manunuzi kwasababu hakuna namna wataepuka matumizi ya mfumo wa NeST. “Nilihudhuria kikao cha ALAT mkoa na suala la mfumo huu ulizungumzwa na kila mkurugenzi na rai yao wote ilikua ni kwamba watumiaji wa mfumo huo wasikae kimya wapatapo changamoto ni vema wakawa na desturi ya kuripoti ili kufanya marekebisho ili mfumo ukae sawa na kuwa rafiki kwa matumizi. Kwahiyo ninaamini kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha mfumo huo unaimarika” alisema Prof. Mwamfupe.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri