Barabara ya Lami ya Kilometa 6 yawanufaisha wakazi wa Kata ya Miyuji
Na. Abdul Juma, MIYUJI
Diwani wa Kata ya Miyuji, Beatrice Ngerangera amesema ujenzi
wa Barabara ya kilometa sita ya kutoka Miyuji hadi Ipagala umesaidia kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi na kuharakisha
usafiri katika mazingira bora na salama.
Kauli hiyo aliiotoa alipokuwa akiwaelezea waandishi wa habari mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka minne katika Kata ya Miyuji.
Ngerangera alisema kuwa kilio kikubwa cha wananchi wa
Miyuji ilikuwa ni barabara. “Nitumie fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utawala wake, Kata ya
Miyuji imepata mambo mengi mazuri hasa ujenzi wa Barabara. Hapo zamani ilikuwa
ni vigumu kupita kwenye barabara hii ila hivi sasa tunapita kwa amani. Mradi wa
barabara hii yenye urefu wa kilomita sita, inaunaganisha kati ya Kata ya Miyuji
na Ipagala. Hivyo, umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.7. Awali wananchi
walikuwa wakipata taabu wakati wa mvua. Mimi, najisikia vizuri, kipekee nimpongeze
mama, rais wa wanyonge kwakuwa amesikia kilio chetu niseme Mungu ambariki sana”.
Akiongelea faida za barabara hiyo alizitaja kuwa ni
kuondoa changamoto ya kina mama kujifungulia njiani. “Hakuna kuharibika kwa
vyombo vya usafiri, pia ajali zimepungia, zamani watu walikuwa wanafia njiani
kwasababu ya ubovu na ufinyu wa barabara wakiwa wanafuata huduma ya afya katika
hospitali ya St. Gemma” alisema.
Nae Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyuji Proper, Hawardi
Mbogela aliipongeza serikali ya awamu ya sita na Mbunge, Anthony Mavunde kwa
kuweza kutimiza ahadi ya kuwajengea barabara yenye kiwango cha lami. “Rais wetu
amekuwa akisikiliza sana kilio cha wananchi wake, sisi kama viongozi wa kata
hii tulikaa pamoja na diwani tukawasilisha suala hili kwenye uongozi wa juu,
hatimae limetekelezwa kwa asilimia miamoja. Hivyo, nimpongeze Rais mama Samia
na mbunge wetu Mavunde bila kusahau Diwani wa Miyuji, Beatrice” alisema Mbogela.
Kwa namana nyingine wakazi wa Kata ya Miyuji waliweza
kueleza ni kwa namna gani wamefurahi kwa kutekelezwa kwa mradi huo wa ujenzi wa
barabara katika kata yao kwasababu mradi huo umekuwa fursa katika kata yao.
Akizungumza mkazi wa Miyuji Proper, Maria Juma
aliishukuru serikali kwa kusikiliza malalamiko yao kwa kuwajengea barabara
iliyowaunganisha na Kata ya Ipagala. “Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwaajili ya barabara
hii. Pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu barabara hii
imetunufaisha sisi wananchi wa Miyuji. Kabla ya barabara hii hali ilikuwa mbaya
hapa katika kata yetu kulikuwa na makorongo hata wananchi wengine walifia
njiani na kujifungulia wakiwa wanaenda katika Hospital ya St. Gemma kupata
huduma,” alisema Juma.
Comments
Post a Comment