Mfumo Jumuishi kutoa mikopo ya 10% Jiji la Dodoma
Na. Nancy Kivuyo, TAMBUKARELI
Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa kushirikiana na Benki ya CRDB wamefanya kikao kazi kuhusu utoaji na
usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia
mfumo jumuishi kwa lengo la kujenga uelewa wa Pamoja kuhusu utoaji wa mikopo hiyo.
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity Sichona |
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity Sichona akizungumza na watendaji wa kata na maafisa maendeleo ya jamii, alisema kuwa kanuni na sheria za utoaji wa mikopo kwa vikundi ni muhimu. Aliwataka wazichukue ili wakatoe elimu ya kutosha katika kufanikisha utaratibu wa kupata mikopo kwa haraka na kwa wakati. “Mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inatekelezwa kwa mujibu wa sheria kwa uwiano wa 4-4-2 ikimaanisha wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili” alisema Sichona.
Aidha, aliwasisitiza
kuzingatia miongozo na sheria za utoaji mkopo lakini pia kwenda kutoa elimu
iliyo sahihi kwa vikundi kwasababu mikopo itatolewa kupitia benki, hivyo,
vikundi vinatakiwa kuwa na akaunti itakayowawezesha kuweka pesa za mkopo.
Nae, Meneja Biashara wa
Benki ya CRDB, Andrew Mwiziwa alizungumzia namna benki hiyo wanashirikiana na
mamlaka za serikali katika kuhudumia vikundi vya wajasiriamali vinavyohitaji
mikopo ya riba nafuu kwa lengo la kujikwamua kiuchumi. Alifafanua kuwa “akaunti
za vikundi hazina makato lengo likiwa ni kuvisaidia vikundi hivyo kuendeleza
miradi yao kwa ufanisi ili wafikie malengo yao” alisema Mwiziwa.
Alisema kuwa viwango vya
ukomo wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu vinaanzia shilingi 500,000 kiwango cha chini na shilingi 150,000,000 kwa
kiwango cha juu.
MWISHO
Comments
Post a Comment