Dodoma Jiji FC, Fiti Kuwavaa Wajelajela
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imejiandaa
kuwakabili Klabu ya soka ya Tanzania Prisons katika muendelezo wa mbilinge
mbilinge za duru ya pili ya Ligi kuu ya NBC Tanzania bara hapo kesho katika
dimba la Jamhuri Dodoma.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa
habari kuelekea mchezo wa Tanzania Prisons, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Meck Mekisime alisema “Timu ipo tayari na
tumejiandaa vizuri tukijua kuwa mchezo utakua mgumu kwasababu wapinzani wetu
wametoka kupoteza michezo miwili mfululizo. Kwahiyo, sisi kama klabu tupo
tayari kupambana na kuhakikisha alama tatu zinabaki Dodoma na niwaombe
mashabiki na wanadodoma kwa ujumla kesho waje kwa wingi uwanjani kuja kuwaunga
mkono wachezaji na kuwafariji kutokana na kile kilichotokea siku kadhaa
zilizopita, jambo ambalo litawaongezea nguvu wachezaji kuipambania timu huku
wakijua kuna namba kubwa ya watu jukwaani inawaunga mkono”.
Nae, Augustin Nsata, Nahodha wa klabu ya
Dodoma Jiji FC, akaelezea hali ya utimamu wa wachezaji kuelekea katika mchezo
huo. “Kama wachezaji morali ni kubwa na tupo salama kiakili na kimwili kuelekea
katika mchezo huo, na kila mchezaji anautaka mchezo na yupo tayari kuipambania
nembo ya klabu, kikubwa tuwaombe mashabiki waje kwa wingi uwanjani kutuunga
mkono vijana wao ili kwa pamoja tuhakikishe tunashinda mchezo huu na kuendelea
kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi na kila mchezo kwasasa
kwetu ni fainali” alisema Nsata.
Kuelekea mchezo huo Dodoma Jiji FC,
imeanzisha kaulimbiu inayoitwa Mchezo wa Shukrani ambapo Dodoma Jiji FC,
itatumia mchezo huo kumshukuru Mungu kutokana wachezaji wake, maafisa na benchi
lake la ufundi kunusurika katika ajali waliyoipata wiki iliyopita wakati timu
ikitokea mkoani Lindi ambapo ilitoka kulazimishwa sare na Namungo FC.
MWISHO
Comments
Post a Comment