Elimu ni haki ya watoto wenye mahitaji maalum Kata ya Ipagala
Na. Coletha Charles, IPAGALA
Halmashauri ya
Jiji la Dodoma imeendelea na jitihada ya utambuzi wa watoto wenye mahitaji
maalum kiafya kwa lengo la kujiunga na elimu ya awali na msingi kwa mwaka wa
masomo 2025 katika Kata ya Ipagala.
Akizungumza wakati
zoezi hilo, Afisa Elimu wa Kata
ya Ipagala, Veronica Mpanda, aliwaomba wazazi kuwapeleka watoto wenye
mahitaji maalum shule kwa sababu wanahaki ya kupata elimu kama watoto wengine
kulingana na sera ya elimu jumuishi kwa kuwa miundombinu imara ipo kwa ajili
yao.
Alisema kuwa zoezi
hilo linalenga kutambua idadi na aina ya mahitaji ya watoto hao ili kuweka
mipango madhubuti ya kuwahudumia. “Zoezi hili la uandikishaji lilitakiwa
lifanyike katika Shule ya Msingi ya Ipagala B, lakini hatujafanikiwa kupata
mtoto hata mmoja mwenye mahitaji maalum japo zoezi hili ni endelevu na
tunatambua kwamba elimu ni haki ya kila mtoto na kupitia zoezi hili
tutahakikisha kuwa hakuna mtoto anayebaki nyuma kwa sababu ya changamoto
yoyote” alisema Mpanda.
Nae, Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Upimaji Shule ya
Msingi Nkuhungu, Deogratias Montano, alisema kuwa
wanawapima na kuwapangia watoto hao shule stahiki ambazo wanaweza kusoma bila
shida na zoezi hilo litaendelea ndani ya wiki mbili.
Alisema kuwa
mwitikio bado siyo mzuri kwa wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalum
japokuwa wamejipanga kutokuacha mtoto nyumbani ambaye ana ulemavu wa macho,
ulemavu wa viungo, mtindio wa ubongo na ulemavu wowote. “Tunashirikiana kwa
karibu na wazazi na walezi wa watoto hawa ili kuhakikisha tunapata taarifa
sahihi. Hii inatusaidia kupanga huduma zinazofaa kulingana na mahitaji ya kila
mtoto na hatua hii ni muhimu kwa maendeleo ya jamii nzima. Elimu inatakiwa
itolewe kwa upana juu ya jamii kuhusu umuhimu wa kuwasaidia watoto” alisema
Montano.
Halmashauri ya Jiji
la Dodoma imejipanga kuboresha hali ya watoto wenye mahitaji maalum kwa
kuhakikisha wanajumuishwa kikamilifu katika mfumo wa elimu na maisha ya kila
siku.
MWISHO
Comments
Post a Comment