Rais, Dkt. Samia aagiza fedha za maadhimisho ya Uhuru kutumika kwenye huduma za kijamii- Majaliwa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Maadhimisho ya
Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Mwaka 2024 yafanyike katika ngazi ya
mikoa na Fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili ya Maadhimisho
hayo zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii.
Amesema kuwa
kila mkoa uhakikishe Wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ikiwemo upandaji
miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile kwenye Masoko,
Hospitali, Kambi za wazee na wenye mahitaji maalum, mashindano ya michezo
mbalimbali pamoja na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu
ambayo nchi yetu imefikia katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru.
Amesema hayo
leo Jumatano (Desemba 04, 2024) katika kikao kazi cha Mawaziri kilichofanyika
katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. “Sherehe za Mwaka huu hazitakuwa na
Gwaride na Shughuli nyingine za Kitaifa”.
Amesema kuwa
Serikali inatoa wito kwa Wananchi kushiriki katika shughuli hizo ili kujivunia
sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru wetu. “Ninatoa rai kwa Wakuu wote wa
Mikoa ya Tanzania Bara, kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo Mahsusi yaliyotolewa
na Serikali ili kuhakikisha Maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo
la kuuenzi Uhuru wetu.”
Ameongeza
kuwa shughuli za Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ya Mwaka
2024 zilishaanza tangu tarehe 02 na zitafanyika mpaka tarehe 09 Desemba, 2024
Siku ya kilele.
“Katika
Maadhimisho haya, Taasisi zote za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na
Usalama zinaelekezwa kuhakikisha Majengo yote ya Serikali Tanzania Bara
yanapambwa kwa vitambaa vya rangi ya Bendera ya Taifa, picha rasmi ya Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni Muasisi wa Uhuru wetu
pamoja na picha ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania”.
Kauli Mbiu
ya Maadhimisho hayo ni: Miaka 63
ya Uhuru wa Tanzania Bara: “UONGOZI MADHUBUTI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI NI
MSINGI WA MAENDELEO YETU.”
Chanzo: https://www.pmo.go.tz
Comments
Post a Comment