Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura Waaswa kuviishi viapo vyao
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wasimamizi
wa vituo vya kupigia kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa kuviishi
viapo vyao walivyoapa ili wawe na muongozo mzuri pindi watakapokuwa katika
vituo vyao vya kazi ifikapo tarehe 27 Novemba, 2024.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko wakati akifungua semina
Hayo
yalisemwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akifungua semina ya wasimamizi wa
vituo vya kupigia kura iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
“Mtaenda
kuapishwa, naomba mkaishi kiapo mtakachokipata, ili iwe dira na ndio yawe
makatazo ya mambo ya kutokufanya wakati wa usimamizi” alisisitiza Dkt.
Sagamiko.
Akiongelea
kuhusu kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, aliwasisitiza
wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, kufuata kanuni za uchaguzi za mwaka huu
2024, kwasababu ni tofauti na kanuni za uchaguzi uliopita. Hivyo, aliwataka
kuwa makini ili wasifanye makosa ifikapo tarehe 27 Novemba, 2024. “Najua wapo
waliowahi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, Naomba niwaambie
tunahitaji kuongeza umakini na usikivu wakati huu wa mafunzo, hata kama ulikuwa
umesimamia mwaka 2019, uchaguzi huu ni wa mwaka 2024 na haujawahi kufanyika
popote, utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024. Na kama ni wafuatiliaji yapo mengi
ya tofauti kati ya chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu. Moja ya
tofauti ni mabadiliko ya kanuni. Kanuni zilizotumika katika uchaguzi wa 2019 na
chaguzi nyingine kabla ya hapo ni tofauti sana na kanuni zinazotumika mwaka
huu. Hivyo, niwasihi muongeze umakini katika kusikiliza ili tusiende kuharibu
siku hiyo. Bahati nzuri wengi wenu ni walimu na miongoni mwenu mlishawahi kusimamia
kazi maalumu na sisi tunasema miongoni mwa mambo ambayo hautakiwi kucheza nayo
mojawapo ni uchaguzi, nafikiri ni miongoni mwa yale mambo makuu ambapo ukipata
nafasi ya kushiriki unakosa usingizi ni pamoja na uchaguzi. Uchaguzi unatoa hatima
ya usalama na utulivu wa taifa letu. Maendeleo ya sehemu yoyote yanategemea
sana hali ya usalama katika eneo husika” alisema Dkt. Sagamiko.
Akiongelea
kuhusu sifa na vigezo vilivyotumika kuchagua wasimamizi wa vituo vya kupigia
kura, alikanusha madai ya kuwa wasimamizi hao walichaguliwa kwa upendeleo. “Leo
mtapata mafunzo mafupi lakini pia zoezi kubwa la kuapishwa, kuwa rasmi kwenda
kusimamia vituo vyetu kwa siku ya uchaguzi. Ninajua wapo wenzenu ambao
waliwauliza kwanini mimi nimekosa na wewe umepataje? wengi wanaweza wakahisi
kwamba kuna watu juu yenu waliofanya muwe hapo lakini niwahakikishie ni sifa
zenu ndizo zilizowafanya muwe hapo” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Aidha,
aliwapongeza wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kwa kuchaguliwa kuwa miongoni
mwa wasimamizi wa vituo siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “Niwapongeze
sana kwa kupata nafasi ya kuteuliwa kuwa miongoni mwa wasimamizi wa vituo siku
ya tarehe 27 Novemba, 2024 kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jiji la
Dodoma lina watumishi takribani 5,000 tano ‘plus’ na mliobahatika
takribani 1,450 na, mnaweza mkaona ni namna gani mchujo ulikuwa mgumu, lakini
niwaambie tu ni kutokana na weledi wenu, sifa zenu na uzalendo wenu kwa taifa
letu, ndio maana leo mpo hapa kwa ajili ya kupata mafunzo mafupi lakini kwa
tukio kubwa kabisa la kuapishwa” alipongeza Dkt. Sagamiko.
MWISHO
Comments
Post a Comment