Juhudi na nidhamu yatakiwa kwa washiriki wa mafunzo ya Jeshi la Akiba Dodoma
Na. Rahma Abdallah, MPUNGUZI
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri amewataka washiriki wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwa muda wote wa mafunzo na kuzingatia yote watakayo fundishwa ili kuwa kuwa askari mahili.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri akifungua mafunzo ya Jeshi la Akiba
Hayo aliyasema wakati akifungua mafunzo ya 17 ya Jeshi
la Akiba Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa michezo wa Shule ya Sekondari
Mpungunzi iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa wakufunzi wa mafunzo
hayo wanauzoefu mkubwa utakaowasaidia kuimarika katika kozi mbalimbali za jeshi
la akiba. “Niwaase mfuate maelekezo, mfuate mafunzo yote ya medani, mafunzo ya kitendaji,
pia kuwa na nidhamu wakati wote wa mafunzo. Msingi mkubwa wa kazi za jeshi ni
nidhamu. Huwezi kuwa askari kama huna nidhamu. Kwahiyo, mtapimwa viwango vyenu
vya nidhamu” alisema Alhaj Shekimweri.
Pia aliongeza kwa kusema “tafsiri ya kwanza ya nidhamu
ni kuheshimiana ninyi kwa ninyi, kuwaheshimu viongozi wenu wa kambi, kuwaheshimu
viongozi wanaokuja kuwatembelea na kuwatia nguvu huku mkitambua kuwa yote
mnayoyafanya ni chini ya mwamvuli wa jeshi la ulinzi na usalama wa nchi yetu”.
Sanjari na hayo aliwasisitiza kujitokeza na kushiriki
katika uboreshaji wa taarifa kwenye daftari la mpira kura pamoja na kushiriki
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba,
2024. “Hakikisheni mnahuisha taarifa zenu na kwa wale ambao walikuwa na umri
mdogo katika uchaguzi uliopita na sasa wamefikia umri wa kushiriki mkajiandikishe.
Ukiona una sifa za kuwa kiongozi, chukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali na
wakati ukifika shiriki kumpigia kura kiongozi atakayekufaa” Alhaj Shekimweri
alisisitiza.
Alihitimisha kwa kuwapongeza washiriki wa mafunzo kwa
utayari wao na uzalendo na kuwatakia heri katika muda wote wa mafunzo. Aidha,
aliwataka wakufunzi wa mafunzo hayo kuwaandaa kikamilifu washiriki hao ili wawe
raia wema kwa nchi yao.
Akiwasilisha taarifa ya mafunzo hayo, SSGT. Lusajo
Mwakanyamale, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Dodoma alisema kuwa washiriki
wa mafunzo hayo wametoka tarafa ya Dodoma mjiji pamoja na Zuzu. Alisema baadhi
yao ni walinzi kutoka makampuni binafsi na wengine ni kutoka kwenye mitaa
wanayoishi kwa mujibu wa sheria. “Afande mgeni rasmi napenda kukuhakikishia
kuwa mafunzo haya yatafikia viwango vinavyokubalika na jeshi la akiba na
watakuwa tayari kulitumikia taifa. Mafunzo haya yatafanyika kwa majuma 18
(miezi 4)” alisema SSGT. Mwakanyamale.
Mafunzo ya Jeshi la Akiba Wilaya ya Dodoma ni mafunzo
ya awamu ya 17 yakilenga kuwajengea washiriki utimamu wa mwili, ukakamavu,
ujasiri na uzalendo kwa taifa lao kupitia masomo mbalimbali ikiwa ni pamoja na usalama
wa raia, huduma ya kwanza, ramani, zimamoto, uhamiaji na elimu ya kupambana na rushwa,
alisema SSGT. Mwakanyamale.
Kwa upande wake Lameck Mashaka, Mshiriki wa mafunzo
hayo alisema kuwa uzalendo kwa nchi ndio msukumo uliomfanya kujitokeza na
kupata mafunzo hayo. Aliahidi kuzingatia mafunzo hayo na kuyafanyia kazi mara
baada ya kuhitimu. “Nashukuru kwa kupatiwa nafasi hii ya ushiriki kwenye haya
mafunzo na imani yangu kubwa nitaimarika na kwenda kuitumikia nchi yangu kwa uzalendo”
alisema Mashaka.
MWISHO
Comments
Post a Comment