Vitengo vya Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Dodoma vyapongezwa kwa utendaji kazi mzuri
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
VITENGO vya Mawasiliano Serikalini katika Mkoa wa Dodoma
vimepongezwa kwa kuhabarisha wananchi juu ya kazi nzuri zinazofanywa na
serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada
ya Mkoa wa Dodoma kushika nafasi ya nne katika utoaji habari nchini kufuatia
tathimini iliyofanywa na Idara ya Habari (Maelezo) chini ya Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari juu ya umahili wa utoaji habari kwa vitengo vya mawasiliano serikalini.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma,
Kaspar Mmuya wakati akipokea zawadi ya kikombe na cheti baada ya Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushika nafasi ya nne kati ya mikoa 26 ya
Tanzania bara.
Mmuya alisema “napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ya
kuhabarisha wananchi juu ya kazi na miradi mbalimbali ya maendeleo
inayotekelezwa katika Mkoa wa Dodoma. Hakika mmemuheshimisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Mheshimiwa Rosemary Senyamule. Nimefahamishwa kuwa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kimeshika nafasi ya nne, Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dodoma kimeshika nafasi ya 13
na Halmashauri ya Mji wa Kondoa nafasi ya 15. Mwaka huu tulioanza tunataka
kupiga hatua zaidi na kushika nafasi ya kwanza kwa sababu Dodoma ndiyo fahari
ya watanzania”.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua katika kukuza uhuru wa habari ili wananchi
waweze kupata habari sahihi. Habari sahihi zinapatikana katika vitengo vya
mawasiliano serikalini. “Nimefurahishwa na umahiri wenu katika kuuhabarisha
umma, matumizi ya mitandao ya kijamii na uhuishaji wa tovuti za serikali. Wito wangu
kwenu endeleeni kujipanga zaidi ili habari na taarifa sahihi ziwafikie wananchi
wengi zaidi” alisema Mmuya.
Kwa upande wake Afisa Utumishi Mkuu katika Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Lucy J. Timba, wakati akikabidhi zawadi ya kikombe na
cheti kwa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, alisema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
na halmashauri zake mbili wamefanya vizuri katika tuzo za umahili wa vitengo
vya mawasiliano serikalini kwa utoaji wa habari kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema kuwa katika tuzo hizo Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kilishika nafasi ya nne na kupewa
zawadi ya kombe na cheti cha utambuzi. “Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmasahuri ya Jiji la Dodoma kilishika nafasi ya 13 na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Halmashauri ya Mji Kondoa kilishika nafasi ya 15 na wote kupewa
zawadi ya cheti cha utambuzi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Hellen Minja alisema kuwa kitengo chake
kimejipanga kupiga hatua zaidi. “Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tunampango wa kufanya vizuri zaidi na kuwa
washindi namba moja katika kuhabarisha umma nchini. Tutafanya kazi zaidi ya
mwanzo ili tuwe bora” alisema Minja.
Tuzo ya umahili wa vitengo vya mawasiliano serikalini
vilivyofanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilitangazwa na Mkurgenzi wa
idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali mbele ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 18 June, 2024 katika Kongamano la pili la maendeleo
ya sekta ya Habari nchini lililohudhuriwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na
zawadi kukabidhiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa
niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 21 June, 2024 katika
ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
MWISHO
Comments
Post a Comment