Mikopo ya Makundi Maalum kurejeshwa Julai, 2024
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu utakaoanza Julai, 2024.
Akiwasilisha bungeni utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2023/24 na
makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka 2024/25, Mchengerwa
mikopo hiyo itaanza kwa utaratibu wa kutumia benki kwa halmashauri 10 za
majaribio ambazo ni Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma Ujiji na Songea, Miji
ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.
Aidha, alisema halmashauri 174 zilizobaki zitatumia utaratibu
ulioboreshwa ili kuondoa mapungufu yaliyosababisha changamoto za awali kwa
kufanya mambo yafuatayo; uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na
uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za ofisi za wakuu wa
mikoa, halmashauri na kata.
“Majukumu ya kamati ngazi ya kata ni kutambua waombaji na
kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili kwenye mfumo kabla ya kuwasilisha
kwenye kamati ya halmashauri, kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kusanifu
na kujenga mfumo mpya unaoitwa Wezesha Portal utakaotumika kwa ajili ya
taratibu za ukopeshwaji wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,
mfumo huu utaondoa changamoto za mfumo zilizokuwepo awali kabla ya mikopo
kusimamishwa,” alisema.
Alisema maboresho mengine yaliyopangwa kufanyika ni kujenga
uwezo kwa wasimamizi wa mikopo hiyo kwa kuongeza idadi ya 91 wasimamizi wa
mikopo kwenye ngazi ya kata ambapo maafisa maendeleo ya jamii 787 wameajiriwa
na kupangiwa kata zilizokuwa na upungufu. Watumishi hao na timu nzima
itakayosimamia mikopo hiyo katika ngazi zote itapatiwa mafunzo na wataalamu
wabobezi wa usimamizi wa mikopo ya aina hiyo.
Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kurekebisha sheria
inayosimamia mikopo hiyo na kanuni zake ili kuongeza ufanisi. Baada ya kipindi
cha mpito, tathmini itafanyika ili kubaini mfumo bora utakaotumika katika
utoaji wa mikopo hiyo.
“Mikopo inayotarajiwa kutolewa ni shilingi Bilioni 227.96 ambapo
Shilingi bilioni 63.67 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa
kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa, shilingi bilioni 63.24 ni
fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na shilingi bilioni 101.05 ni
fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya
mwaka 2024/25.
Comments
Post a Comment