Kata ya Chamwino kipaumbele Lishe shuleni

Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO

KATA ya Chamwino imetoa kupaumbele katika agenda ya lishe ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na lishe bora na kuendelea na masomo yao vizuri.


Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alipokuwa akiongea na walimu, wanafunzi na wadau wa masuala ya lishe katika Shule ya Msingi Chamwino iliyopo katika Kata ya Chamwino, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

“Leo ni maadhimisho ya kidunia kuhamaisha matumizi ya mimea jamii ya mikunde. Kama maharage, njegere, choroko, mbaazi. Sisi Kata ya Chamwino suala la lishe lina umuhimu mkubwa sana. Lengo ni kupinga hali ya udumavu, ukondefu na athari zote zinazotokana na lishe duni. Kata ya Chamwino tumeweka mikakati mizuri kuhakikisha wanafunzi katika shule zetu tatu za msingi na moja ya sekondari wanaweza kupata chakula shuleni. Na leo hapa tumekuja Shule ya Msingi Chamwino yenye wanafunzi takribani 2,500 kuhamasisha lishe. Na hii shule inafanya vizuri katika utoaji wa chakula shuleni, inafikia asilimia 92. Shule inatoa uji kwa madarasa ya awali na chakula cha mchana kuanzia darasa la tatu hadi la saba” alisema Nkelege.

Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt. Honest Kessy alisema kuwa maadhimisho ya siku ya kula mazao ya mikunde kuna lenga kuhamasisha ulaji wa vyakula vyenye virutubishi mwilini. “Wanafunzi mpende kula maharage na muwashawishi wazazi waweze kuwapikia maharage na mboga jamii ya mikunde. Vyote hivi vyakula vinaumuhimu sana kwa sababu vinatuongezea virutubishi katika miili yetu, vinaongeza uwezo wetu wa kufikiri na kuelewa darasani. Niwaombe sana tusipuuze vyakula vinayotokana na jamii ya mikunde” alisema Dkt. Kessy.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Shule ya Msingi Chamwino, Mwl. Ezekiel Lenjima alisema kuwa shule hiyo imefurahia zoezi la upandaji wa mbogamboga. “Kwa niaba ya Shule ya Msingi Chamwisho niwashukuru viongozi wa serikali, sekta binafsi na waendesha baiskeli kufanya kilele cha maadhimisho haya katika shule yetu. Tuwahakikishie kwamba mbegu hizi za mboga tulizopanda shuleni hapa tutazitunza, tutazimwagilia na mavuno yake yatatusaidia sana katika kuchanganya mboga kwenye maharage. Maharage tunayotumia kwa chakula katika shule yetu yatakuwa yameongezewa virutubishi vitakavyoongeza lishe kwa wananfunzi wetu na kukuza uwezo wao wa kiakili” alisema Lenjima.

Zoezi la kusia mbegu za mboga katika Shule ya Msingi Chamwino lilitanguliwa na mbio za baiskeli zilizolenga kuhamaisha afya bora dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambuza na kuchochea masuala ya lishe bora kwa jamii.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma