MKOA WA DODOMA WAPATA HATI SAFI KATIKA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2023
Na. Mwandishi Maalum, KITETO
Mkoa wa Dodoma wapata hati safi katika mbio za Mwenge wa Uhuru
mwaka 2023 baada ya miradi yake 45 kukubaliwa na katika wilaya saba na
halmasahuri nane za mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akitoa taarifa ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Mkoani Dodoma
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary
Senyamule leo tarehe 7 Oktoba, 2023 wakati akikabidhi Mwenge wa Uhuru
2023 kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga katika uwanja wa Shule ya
Msingi Dosidosi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto.
Senyamule akitoa taarifa ya hitimisho kwa mbio za Mwenge wa
Uhuru 2023 kwa Mkoa wa Dodoma, alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa kwa
takribani kilometa 1893 na kupitia jumla ya miradi ya maendeleo 45.
Miradi 15 iliwekewa jiwe la msingi, miradi 19 ilizinduliwa na 11
ilitembelewa yote ikiwa na jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi Billioni 16.
Miradi hiyo ni pamoja na miradi ya sekta za elimu, afya na miradi ya utunzaji
wa Mazingira aliongeza.
Aidha, alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ulipita katika wilaya zote
saba na Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma ambazo ni Bahi, Chemba,
Kondoa DC, Kondoa Mji, Dodoma Jiji, Chamwino, Mpwapwa na kumaliza mbio zake
kwenye Wilaya ya Kongwa.
"Dada yangu Queen Sendiga na viongozi wote mliokusanyika
hapa nitumie fursa hii kuwatangazia na kuwajulisha kwamba, miradi yote 45
katika Mkoa wa Dodoma ilipita salama bila kukataliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru
2023. Hivyo, niwapongeze sana wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu 2023
kwa kazi hii iliyotukuka mlioifanya Dodoma" alieleza Senyamule.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, aliahidi kutekeleza
maelekezo kwa sehemu zote ambazo viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru walishauri
kufanyiwa marekebisho na mkoa utahakikisha maeneo hayo yanaboreshwa.
Kwa Upande Wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga wakati
akipokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisema kuwa Mwenge wa
Uhuru utakapo kuwa mkoani kwake utatembelea miradi ipatayo 57 yenye thamani ya
jumla ya shilingi Billioni 13.2, utaweka jiwe la msingi, utazindua na kukagua
miradi mbalimbali.
Nae, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Abdalla
Shaib Kaim aliupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kupata hati safi katika miradi yote
iliyokaguliwa na Mwenge wa Uhuru huku akifurahishwa na ushirikiano uliooneshwa
na viongozi katika kipindi chote Mwenge wa Uhuru ulipokua ndani ya Mkoa huo.
MWISHO
Comments
Post a Comment