WAKAZI WA KATA YA NALA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA KABLA YA SAA 10 JIONI
Na. Theresia Nkwanga, NALA
MSIMAMIZI
wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, John Kayombo amewataka wakazi wa Kata ya
Nala kujitokeza na kutumia haki yao ya kidemokrasia kupiga kura kumchagua
mwakilishi wao.
![]() |
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, John Kayombo akimsikiliza mpiga kura katika moja ya kituo cha kupigia kura Kata ya Nala |
Kayombo
alisema hayo katika kituo cha Sengu chini apokuwa akitoa muhtasari wa hali ya
uchaguzi mdogo wa Diwani Kata ya Nala unaoendelea katika vituo 12 vya kata
hiyo.
“Leo tarehe 19
Septemba, 2023 Kata ya Nala inafanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya aliyekuwa
Diwani aliyefariki. Zoezi la kufungua vituo lilifanyika kama sheria inavyotaka
saa 1:00 asubuhi. Mpaka sasa saa 6 mchana zoezi la upigaji wa kura linaendelea
vizuri na wananchi wamejitokeza kwa wingi kuja kuchagua mwakilishi wao. Niwaombe
wananchi waendelee kujitokeza muda bado sasa ni saa 6 mchana hadi saa 10 jioni ndio
tunafunga vituo” alisema Kayombo.
Aidha,
aliwataka wananchi wakimaliza kupiga kura kurudi nyumbani. "Vituo vya
kupiga kura baadae vinabadilika kuwa vituo vya kuhesabia kura. Mwisho matokeo
ya kila kituo yatabandikwa kwenye mbao za matangazo kwa kila kituo. Baada ya
zoezi hilo, wasimamizi wote wataondoka kuja kwenye kituo cha majumuisho ya
vituo vyote kwenye Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Nala. Mshindi wa kiti cha Diwani
Kata ya Nala atatangazwa leo na cheti cha ushindi kitatolewa leo” alisisitiza
Kayombo.
Kuhusu
hali ya upigaji kura, alisema kuwa wananchi wanapiga kura katika hali ya amani
na utulivu. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imejipanga vizuri kabisa.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa,
Mhe. Mwanaisha Kwariko alisema kuwa hali ya vituo vya kupigia kuwa ni nzuri na
vifaa vyote vilifika mapema na watendaji wote walikuwepo na ilipofika saa 1:00
asubuhi watendaji walikuwa tayari kuwapokea wapiga kura.
“Katika
vituo vingi tulivyotembelea wapiga kura wengi walikuwa wameshafika kwa ajili ya
zoezi hilo na wananchi walikuwa wakifuata maelekezo ya kujipanga kwenye mistari
kwa ajili ya kupiga kura kwa utaratibu. Muitikio wa watu ni mzuri wa watu
kishapiga kura wanaondoka. Hata wenye mahitaji maalum wanapokelewa na
kuhudumiwa kama tulivyoelekeza wanapiga kura mapema na kuondoka” alisema Mhe. Kwariko.
Nae
Mratibu wa Uchaguzi, Albert Kasoga alisema kuwa walijiaandaa vizuri kwa vituo
vyote 12. “Kwa upande wa wasimamizi maandalizi yalifanyika na wote walipata
mafunzo na wapo vizuri na wapo vituoni kama maelekezo yalivyokuwa” alisema
Kasoga.
Mkazi
wa Mtaa wa Chiwondo, Samwel Kusalo alisema kuwa zoezi hilo limeratibiwa vizuri.
“Tulitangaziwa leo ni siku muhimu ya kutumia haki yetu ya msingi kupiga kura
kumchagua diwani wetu. Nimekuja, nimepokelewa vizuri na wamekagua wakaona jina
langu na nikatumia haki yangu ya msingi kupiga kura” alisema Kusalo.
Kata ya Nala yenye jumla
ya wapiga kura 3,741 na vituo 12 vya kupigia kura inafanya uchaguzi mdogo
kufuatilia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo Julius Chimombo aliyefariki tarehe
10 Aprili, 2023 huku vyama vinavyoshiki uchaguzi huo vikiwa 11.
MWISHO
Picha za Matukio mbalimbali Msimamiz wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma Mjini, John Kayombo akifuatilia maendeleo ya upigaji kura katika vituo
Comments
Post a Comment