WAFANYABIASHARA SOKO LA SABASABA WAHAKIKISHIWA KUFANYABIASHARA HADI MWISHO MWAKA WA FEDHA 2023/2024
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kimewahakikishia wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba
kuwa hawataondolewa katika soko hilo hadi Mwezi Julai mwakani ili waendelee
kutekeleza majukumu yao bila wasiwasi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa katika mkutano
wa hadhara na wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba jijini Dodoma.
Kimbisa
alisema “napenda kuwafahamisha kuwa hadi mwezi Julai mwakani hakuna
mfanyabiashara atakayebughudhiwa hadi halmashauri itakapopata fedha za
kuendeleza soko hilo. Halmashauri wakipata fedha hizo lazima tukae pamoja na
kukubaliana wanaanza na jambo gani na kuendelea na jambo gani. Tunafahamu jiji
mtajenga kwa awamu, mtashirikiana na uongozi wa soko ili kuhakikisha huduma
zinakuwa bora”.
Akiongelea
daladala kuingia katika Soko la Sabasaba, alisema kuwa soko hilo siyo stendi ya
daladala. “Daladala zinapopaki kwa sasa si sawa. Daladala zilipo zitaua watoto
wa shule na wagonjwa. Fanyeni haraka daladala zipite na kushusha na kupakia
abiria katika Soko la Sabasaba hii siyo stendi. Latra kaeni na uongozi wa soko
kuhakikisha daladala zinapita hapa”.
Aidha,
aliutaka uongozi wa soko kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa
kutandaza hadi eneo ambalo daladala zinapita. Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Dodoma
kuhakikisha Askari Polisi wanakuwepo muda wote ili daladala zisitumie muda
mrefu kusubiria abiria.
Kwa
upande wa mfanyabiashara katika Soko la Sabasaba, Madimilo Mbogoni alisema kuwa
walikuwa na hofu ya kuondolewa katika soko hilo. “Tunamshukuru Mwenyekiti wa CCM
kwa kufika kuongea na sisi wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba. Sasa tulikuwa
na hofu kubwa kuhusu kuondolewa katika maeneo haya tumeteseka kwa muda mrefu
kujua hatima yetu. Lakini leo tumepata ufumbuzi na kweli tunawashukuru viongozi
wote walioshiriki mpaka kuhakikisha tumefikia hapa. Hofu yetu imetutoka na
tunamshukuru Mungu” alisema Mbogoni.
MWISHO
Comments
Post a Comment