JIJI LA DODOMA LATUMIA MIL. 23 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetumia zaidi ya shilingi milioni 23 kwa
ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo fedha kutoka serikali kuu, mapato ya
ndani na wahisani pamoja na bakaa.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi kufikia Machi,
2026 halmashauri imetumia jumla ya shilingi 23,815,713,415.02 sawa na asilimia
91.19 ya fedha zilizopokelewa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo. “Kati ya fedha hizo, shilingi 6,406,582,002.56 ni fedha kutoka
serikali kuu, shilingi 16,807,859,627.46 mapato ya ndani, shilingi
601,771,785.00 fedha za wahisani na shilingi 5,279,467,344.52 ni fedha za bakaa. Kwa
kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi kufikia Machi, 2026, halmashauri imepokea
jumla ya shilingi 25,314,611,746.31 sawa na asilimia 55.99 ya makisio yote
ya fedha za miradi ya maendeleo, kiasi cha shilingi 7,139,598,162.00 ni fedha za serikali kuu,
shilingi 814,771,785.00 ni
fedha za wahisani na shilingi 17,360,241,799.31 ni fedha kutoka
mapato ya ndani” alisema Fungo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya TAMISEMI, Florian Kyombo aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa
fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika halmashauri.
Vilevile, alilipongeza Jiji la Dodoma kwa kutenga fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Mwaka wa Fedha 2025/26, katika Mpango na Bajeti ilikadiria kutumia jumla ya shilingi 45,209,805,500.00 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha. Kati ya fedha hizo, shilingi 4,303,552,000.00 ni fedha za wahisani, shilingi 10,074,637,000.00 ni fedha kutoka serikali kuu na shilingi 30,951,616,500.00 ni fedha kutoka mapato ya ndani ambazo ni sawa na asilimia 68.46 ya bajeti ya miradi ya maendeleo.
MWISHO
Comments
Post a Comment