JIJI LATEKELEZA MKAKATI WA KUBORESHA MAENEO YA WAZI
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatekeleza mkakati wa
uboreshaji maeneo ya wazi kwa kusimamia udhibiti na usimamizi wa sheria na
kufanya uondoaji wa maendelezo ya kudumu yaliyokiuka masharti na kuboresha
miundombinu ya maeneo ya michezo.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alipokuwa akisoma taarifa ya uboreshaji wa maeneo ya wazi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliyofanya ziara katika jiji hilo.
Fungo alisema kuwa halmashauri ilifanya zoezi la
mapitio ya hali ya maeneo ya wazi ili kubaini kama yanatumika kwa mujibu wa
sheria. “Halmashauri inatekeleza mkakati wa udhibiti na usimamizi wa
sheria katika maeneo ya wazi, zoezi la uondoaji wa maendelezo ya kudumu
yaliyokiuka masharti ya uendelezaji limefanyika katika eneo la wazi lililopo
Majengo maarufu kama kwa Kato, eneo la Rose Garden na maeneo mengine 47 ambayo
tayari wameshatumiwa ilani yakuondoa maendelezo. Ulinzi na uhifadhi wa
mazingira. Halmashauri katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 inakusudia kupanda miti
ya matunda na vivuri katika maneo ya wazi. Baadhi ya maeneo miti imeshapandwa
mfano, eneo la Chako ni chako na Ukanda wa Kijani UDOM. Mkakati mwingine ni
kuanza utekelezaji wa kuboresha eneo la majengo maarufu kwa Kato na eneo la
Medeli ambayo tayari usanifu wa michoro wa maeneo hayo umeshafanyika na kiasi
cha fedha kutengwa kwa ajili ya uboreshaji. Mwisho kuboresha miundombinu ya
maeneo ya michezo. Halmashauri katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 imetenga fedha
kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya michezo. Mfano, eneo la Chinangali Park
ambapo uboreshaji wake umeanza na unaendelea” alisema Fungo.
Alisema kuwa baada ya taarifa ya maeneo ya wazi, halmashauri iliwasilisha taarifa hiyo katika vikao vya kisheria ambavyo ni Kamati ya Mipnago Miji, Kamati ya Fedha na Utawala na Mkutano wa Baraza la Madiwani wa robo ya pili 2025/2026.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya TAMISEMI, John Nzilanyingi alisema
kuwa halmashauri bado ina jukumu kubwa la kuhakikisha inasimamia na kulinda
maeneo ya wazi kwa maslahi mapana ya wananchi.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inamiliki maeneo ya wazi
katika kata mbalimbali kwa mujibu wa sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 1956
iliyoitwa ‘Town and Country Planning Ordinance’ Sura Namba 378 na kufanyiwa
marekebisho Mwaka 2002.
MWISHO
Comments
Post a Comment