JIJI LA DODOMA LATOA VIWANJA 1,900 KWA WAFANYAKAZI
Na.
Mwandishi wetu, DODOMA
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imeibuka kivingine katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani
kwa kuachia viwanja zaidi ya 1,900 vya matumizi mbalimbali kwa ajili ya
wafanyakazi na wananchi kwa ujumla ili waweze kufurahia fursa ya kumiliki
kiwanja katika makao makuu ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya Halmashgauri ya Jiji la Dodoma katika kujali makazi ya wafanyakazi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika ngazi ya mkoa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Nitumie
nafasi hii kuwashauri na kuwashawishi wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma na wengine wote kuhakikisha wananunua viwanja katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma. Hii itaweka alama kwa utumishi wao katika halmshauri, lakini kwa
wale walio nje ya halmshauri itaweka alama kwa kumiliki kiwanja kihalali katika
makao makuu ya nchi. Wote tu mashahidi kwamba kila mtanzania anatamani awe
sehemu ya makao makuu, wakati uliokubalika ni sasa. Ardhi haiongezeki, ila
inapanda thamani kila uchwao. Natamani kupitia Meimosi hii ya Mwaka 2026, kila
mfanyakazi aweke alama kwa kununua kiwanja katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
makao makuu ya nchi. Na alama hii ili iwe kumbukumbu kwa wengi, mshawishi hata
mwenzako ambae siyo mfanyakazi kununua kiwanja. Pamoja na kuweka alama, pia ni
kuunga mkono maono ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kupitia
kaulimbi ya Dodoma ni fahari ya watanzania” alisema Gondwe.
Akiongelea
mchakato wa kununua viwanja hivyo, alisema kuwa serikali kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu Tamisemi imerahisisha mchakato huo. “Sasa hakuna sababu ya kupanga
foleni kwa ajili ya kununua kiwanja, hakuna sababu ya kusafiri kwa ajili ya
kuja Dodoma kununua kiwanja. Ingia www.tausi.tamisemi.go.tz
jisajili na tafuta Halmashauri ya Jiji la Dodoma nunua kiwanja. Hata mchakato
wa upatikanaji wa hati umerahisishwa, utaingia e-ardhi na kufanya maombi ya
hati mahali popote ulipo. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeachia viwanja zaidi
ya 1,900 vya makazi, biashara, makazi na biashara, taasisi na viwanda katika
maeneo ya Nala, Mahomanyika na Kikombo kwa ajili ya watanzania kuvinunua”
alisema Gondwe.
Kwa
upande wake Mfanyakazi hodari zaidi ya mara moja kutoka Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Theresia Nkwanga alisema kuwa ni
heshima kwa mfanyakazi kumiliki kiwanja katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Ukuaji wa makao makuu ya nchi Dodoma ni wa kasi kubwa. Hivyo, fursa zilizopo
katika ardhi hazina mjadala mpana. Ni kumbukumbu nzuri kwa mfanyakazi na kizazi
chake kuwa historia na sehemu ya mafanikio ya Dodoma kwa kumiliki kiwanja
halili sasa. Hakika Jiji la Dodoma limekuja kivingine” alisema Nkwanga.
Maadhimisho
ya Meimosi mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kazi zenye Staha ni Nguzo imara kwa Maendeleo Endelevu katika
utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050”.
MWISHO
Comments
Post a Comment