Ofisi ya Waziri Mkuu yathibitisha nyenzo muhimu za kuimarisha usimamizi wa maafa nchini
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
SERIKALI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha
mifumo ya usimamizi wa maafa nchini ili kuongeza uwezo wa kuzuia, kujiandaa,
kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa, kufuatia kuongezeka kwa matukio
yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na vihatarishi vingine vya
asili na kijamii.
Hayo yalielezwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya
Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye
Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, wakati akifungua Kikao cha Jukwaa la
Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa kilicholenga kupitia na kuthibitisha
Mwongozo wa Urejeshaji Hali Baada ya Maafa, Mwongozo wa Uendeshaji na Uratibu
wa Uhawilishaji Fedha kwa Walioathirika wa Maafa, pamoja na Mfumo wa Usimamizi
wa Taarifa za Maafa (DMIS).
Brigedia Jenerali Ndagala alisema kuwa katika miaka ya hivi
karibuni Tanzania imekumbwa na matukio mbalimbali ya maafa yakiwemo mafuriko,
ukame, maporomoko ya ardhi, upepo mkali, magonjwa ya mlipuko na ajali
mbalimbali, hali ambayo imeathiri maisha ya wananchi, miundombinu, mazingira na
shughuli za kiuchumi.
“Kwa kuzingatia hali hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu
imeendelea kuimarisha sera, mifumo, mikakati, mipango na nyenzo mbalimbali za
usimamizi wa maafa ili kuhakikisha hatua zote za kuzuia, kujiandaa, kukabiliana
na kurejesha hali baada ya maafa zinafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia
matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022,” amesema.
Alisema kikao hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha uratibu wa
kitaifa wa usimamizi wa maafa kwa kuwa kinahusisha uthibitishaji wa nyenzo tatu
muhimu zitakazochangia uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma
kwa wananchi wakati wa maafa na baada ya maafa.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Ndagala, Mwongozo wa Urejeshaji
Hali Baada ya Maafa utaweka mfumo wa pamoja wa kitaifa wa kupanga na kuratibu
shughuli za urejeshaji baada ya maafa, huku Mwongozo wa Uhawilishaji Fedha kwa
Walioathirika wa Maafa ukiboresha utaratibu wa utoaji wa misaada ya fedha kwa
waathirika. Aidha, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Maafa (DMIS) utaimarisha
ukusanyaji, uchambuzi, uhifadhi na matumizi ya taarifa za maafa kwa ajili ya
kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
“Nyenzo hizi zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Sheria ya
Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 kwa kuimarisha usimamizi wa taarifa,
uratibu wa wadau, utoaji wa misaada na shughuli za urejeshaji hali baada ya
maafa. Vilevile, zinachangia utekelezaji wa Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Hatari
za Maafa kwa kuimarisha uelewa wa hatari za maafa, usimamizi wa vihatarishi,
uwekezaji katika ustahimilivu na kuimarisha hatua za kujiandaa na kujenga upya
kwa ubora zaidi baada ya maafa,” alisisitiza.
Alieleza kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya
usimamizi wa maafa nchini yanatokana na ushirikiano madhubuti kati ya Serikali
na wadau wa maendeleo, mashirika ya Umoja wa Mataifa, sekta binafsi na asasi za
kiraia.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Judith Bihondwa, amesema shirika hilo
litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uwezo wa jamii
kukabiliana na maafa pamoja na kujenga ustahimilivu dhidi ya majanga
mbalimbali.
Amesema ushirikiano huo utaendelea kulenga kuimarisha mifumo ya
maandalizi, mwitikio na urejeshaji hali baada ya maafa kwa kuzingatia makundi
yote ya jamii, hususan watoto na watu walio katika mazingira hatarishi.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa usimamizi wa
maafa kutoka taasisi za Serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za
kiraia na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili na kuthibitisha nyenzo
zitakazochangia kuimarisha usimamizi wa maafa na kuongeza ustahimilivu wa jamii
nchini.
= MWISHO =
Comments
Post a Comment