Kamati ya Kudumu Uchumi, Elimu na Afya yapata Jembe!
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
DIWANI wa Viti Maalum, Joan Mazanda aliibuka kidedea
kwa kupata kura 15 na kuongoza Kamati ya kudumu ya Uchumi, Elimu na Afya katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Uchumi, Elimu na Afya, Joan Mazanda
Akitangaza matokeo hayo, Mstahiki Meya wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alisema kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu
ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Uchumi, Elimu na Afya ni Joan Mazanda.
“Kamati ya kudumu ya Uchumi, Elimu na Afya ilikuwa na wagombea watatu wa nafasi
ya mwenyekiti. Matokeo yalikuwa ni kama ifuatavyo. Mheshimiwa Andrew Muholo,
Diwani wa Ipala alipata kura tatu; Mheshimiwa Fatuma Zollo, Diwani wa Viti Maalum
alipata kura nne na Mheshimiwa Joan Mazanda, Diwani wa Viti Maalum alipata kura
15. Hivyo, mshindi ni Mheshimiwa Joan Mazanda” alisema Chaula.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Madukani,
Prof. Davis Mwamfupe alitoa pongezi kwa Diwani Mazanda kwa kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Uchumi,
Elimu na Afya. “Nampongeza sana kwa nafasi hiyo aliyochaguliwa kwa kura nyingi zaidi,
ni imani yangu kuwa atawajibika kwa weledi mkubwa katika kuhakikisha
upatikanaji wa miundombinu bora ya elimu na afya inastawi na kuwapa wananchi
huduma bora. Lakini pia, eneo la uchumi sina shaka nalo nina amini atalisimamia
kikamilifu” alipongeza.
Nae, Diwani wa Kata ya Mtumba, Ringo Iringo alieleza
furaha yake baada ya baraza kuundwa na kamati za kudumu kupata viongozi wenye
weledi. “Sasa tunaenda kuwatumikia wananchi wa majimbo yetu mawili yaani Dodoma
Mjini na Mtumba. Viongozi wenzangu tuwaunge mkono waliochaguliwa katika nafasi
zote ili kazi ya kuwatumikia wananchi ifanikiwe” alieleza.
MWISHO
Comments
Post a Comment