Diwani Gombo kuongoza Kamati ya Mipango Miji na Mazingira
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Diwani wa Kata ya Ipagala, Gombo Dotto apata ushindi mnono
nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mipango
Miji na Mazingira kwa kuibuka na kura 20 akiwaacha kwa mbali wagombea wawili.
Akitangaza matokeo ya nafasi ya Mwenyekiti, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, alisema kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mipango Miji na Mazingira ni Mheshimiwa Gombo Dotto. “Kamati ya kudumu ya Mipango Miji ilikuwa na wagombea watatu wa nafasi ya mwenyekiti. Mheshimiwa Leonard Ndama, Diwani wa Kata ya Nzuguni alipata kura moja, Mheshimiwa Theobalt Mahina, Diwani wa Kata ya Ntyuka alipata kura moja na Mheshimiwa Gombo Dotto alipata kura 20” alitangaza Mstahiki Meya Chaula.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj
Jabir Shekimweri aliwapongeza viongozi wote waliochaguliwa katika nafasi za
kamati za kudumu na kuwaasa kutumia nafasi hizo kuhakikisha wanasimamia vizuri
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inaenda kuwagusa wananchi moja kwa
moja.
Aliongeza kuwa, eneo la mipango miji na mazingira
linatakiwa kuangaliwa kwa umakini mkubwa ili miundombinu na mazingira ya jiji yawe
katika mpangilio unaovutia. “Tunawategemea kamati hii mtafuatilia na kushauri
kwa umakani namna ‘masterplan’ ya jiji letu inavyotakiwa kuboreshwa zaidi.
Tunatamani kuona jiji likipangiliwa vizuri na miundombinu ionekana kwa nafasi
ili hata wanapokuja wageni, wavutiwe na mazingira rafiki watakayokutana nayo”
aliongeza Alhaj Shekimweri.
Nae, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Mipango Miji na
Mazingira, Gombo Dotto alitoa shukrani zake kwa kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
“Niseme kwamba, nafasi hii nilichaguliwa ni adhimu na nitakwenda kuitumikia
vema. Nawapongeza pia viongozi wenzangu waliochaguliwa katika kamati za kudumu,
tukashirikiane ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli” alishukuru.
MWISHO
Comments
Post a Comment