Wananchi waitwa kupima magonjwa yasiyoambukiza bure Nyerere Square
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza Mkoa wa Dodoma,
Dkt. Missana Yango amewataka wananchi jijini Dodoma kujitokeza kwa wingi
kushiriki katika zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza linaloambatana na
utoaji wa elimu ya afya kuhusu magonjwa mbalimbali.
Alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika bustani ya mapumziko Nyerere Square, ambapo maadhimisho hayo ya wiki ya upimaji wa magonjwa yasiyoambukizwa yakiendelea jijini Dodoma.
Alisema kuwa huduma hizo zinatolewa bila malipo na
zinahusisha upimaji wa magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, saratani,
magonjwa ya moyo pamoja na utoaji wa elimu ya lishe bora na mtindo wa maisha
wenye afya. “Lengo letu ni kuwafikia wananchi wengi kadri iwezekanavyo, ili
wajitambue kiafya na kuchukua hatua mapema kabla magonjwa haya hayajawa sugu.
Huduma zote tunazotoa hapa ni bure, hivyo tunawahimiza wananchi wajitokeze kwa
wingi” alisema Dkt. Yango.
Aliongeza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za
serikali kupitia Wizara ya Afya na ofisi ya Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma
katika kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa
yakiongezeka kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha.“ Lengo la Serikali ni
kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama kiafya pia magonjwa yasiyoambukiza
yanaongezeka kwa kasi, hivyo ni muhimu kila mmoja wetu achukue hatua mapema”
alisema Dkt. Yango.
Nae, Mkazi wa Nzuguni ambae alichangia damu na
mnufaika wa matibabu, Tumaini Shauri alipongeza juhudi hizo zinazofanywa na
serikali akisema zimekuwa zikiwasaidia kutambua hali zao za afya na kupata
ushauri wa kitaalam. “Kwa kweli nashukuru sana serikali kwa kuliona hili na
kutuletea huduma hizi bure katika halmashauri ya Jiji la Dodoma. Nilivyosikia
tangazo hili nikaona nije nipime magonjwa yote yaliyotangazwa na nimefanikiwa,
pia nimepewa ushauri na madaktari, lakini pia niwahamaishe wananchi wenzangu
kujitokeza katika zoezi hili kwasababu ni bure” alisema Shauri.
Zoezi hilo linatarajiwa kuendelea kwa siku tatu na
kuhitimishwa tarehe 14 Novemba, 2025.



Comments
Post a Comment