Changia Damu kuokoa maisha
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Wananchi wahimizwa
kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wale wanaopata dharura ya kuhitaji huduma
ya kuongezewa damu.
Hamasa hiyo ilitolewa
na Mkuu wa Timu za Ukusanyaji Damu Kanda ya Kati, Dr. Leah Kitundya katika
kliniki ya upimaji wa bure wa magonjwa yasiyoambukiza inayoendelea katika
bustani ya mapumziko Nyerere Square jijini Dodoma.
Alisema kuwa kila
mwananchi anawajibu wa kuchangia damu kwasababu inasaidia wakati wa uhitaji.
"Wananchi mliopo hapa Nyerere Square tunawaomba na kuwakumbusha kuchangia
damu kwasababu itatusaidia sote wakati wa uhitaji. Damu yako inaweza kumsaidia
mtu ambae hukutegemea ingemfikia. Changia kuboresha afya za wengine"
alisema Dr. Kitundya.
Aliwaita wananchi
kuchangia damu huku akiwakumbusha kujitokeza kwa wingi kujitolea kwasababu
zinapotokea ajali ama dharura za kuhitaji damu kwaajili ya kuokoa maisha wapo
pia ndugu na jamaa wa karibu wanaweza kukumbwa na kadhia hiyo.
"Ndugu zangu,
uhitaji wa damu ni wa kila mmoja wetu, ukiona leo hii hakuna umuhimu wa
kuchangia damu kesho ndugu yako anaweza kupata ajali au yupo anajifungua
ameishiwa damu ikawa changamoto na majuto kupata msaada wa haraka. Lakini
ukichangia unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuhakikisha wapendwa wako wanapata
huduma bora na ya haraka ya kupata damu pale inapohitajika" alisema Dr.
Kitundya.
Kwa upande wake,
Balozi wa Taasisi ya Magonjwa yasiyoambukiza (NCD), Lawrence Malima ambae
pia ni Msanii wa Bongo Fleva aliungana na wataalam wanaotoa elimu kuwasisitiza
wananchi kutengeneza utamaduni wa kupima afya ili kugundua maradhi yanayowasumbua
huku akichombeza na nyimbo za hamasa. "Kliniki hii ni muhimu kwasababu
itawasaidia kufahamu ni magonjwa gani yanawasibu. Lakini hata wale ambao tayari
wanaugua watapata huduma za awali hapa na watajua hali zao zinaendeleaje.
Nawapongeza sana wananchi wenzangu kwa kuja kupata huduma hizi muhimu.
Mnaochangia damu tunawapongeza hili mnalofanya ni jema na la kuigwa"
alisema.
Nae, Mkazi wa Nzuguni
na mchangiaji wa damu, Tumaini Shauri alipongeza ujio wa kliniki za matibabu ya
bure mara kwa mara na kuishauri serikali kufanya jambo hilo kuwa endelevu.
MWISHO


Comments
Post a Comment