Sungura kitoweo cha gharama nafuu

‎Na. Mwandishi Wetu, HOMBOLO MAKULU


‎Maadhimisho ya Wiki ya Lishe katika Jiji la Dodoma yafanyika kupitia zoezi la ugawaji wa Sungura kwa kaya zenye kipato cha chini kwa lengo la kuzisaidia kupata makundi yote ya chakula bila kuathiriwa na kipato kidogo walichonacho.




‎Maadhimisho hayo yalianza tarehe 17 Novemba, 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa leo tarehe 21 Novemba, 2025.

‎Akizungumza na waandishi wa habari katika zoezi hilo lililofanyika Kata ya Hombolo Makulu, Daktari wa Mifugo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dr. Innocent Kimweri alisema kuwa ufugaji wa Sungura hauna gharama ya kuwatunza na ni kitoweo kizuri kwaajili ya lishe bora.

‎Aliongeza kuwa, suala la lishe wanalihamasisha katika kaya zenye kipato cha chini ili kuwapa elimu ya kutosha kufahamu makundi muhimu ya chakula. "Suala la lishe ni mtambuka, pamoja na kwamba sisi ni maafisa mifugo, tunazingatia ulaji wa mlo kamili. Sungura ni rahisi kutunza kwasababu wanakula tu majani, mabaki ya vyakula na hata nyasi kavu" aliongeza Dr. Kimweri.

‎Dr. Kimweri alimalizia kwa kueleza kuwa utekelezaji wa zoezi hilo hufanyika kila mwaka na ni endelevu. "Tuna utaratibu wa kugawa sungura hawa kwa kuandikishana mkataba baina ya sisi halmashauri na mwananchi anayepewa sungura hao. Tunagawa jike na dume kwa kila mtu lengo likiwa ni kuhakikisha mbegu inapatikana na wanapozaliwa na yeye anagawa kwa kaya nyingine. Kwahiyo baadae jamii nzima inapata sungura ambao ni kitoweo kizuri" alimaliza.

‎MWISHO

Comments

Popular Posts

Agenda ya Lishe yaongeza Ari ya usomaji S/M Dodoma Makulu

Miaka minne ya Dkt. Samia, Kizota yanufaika mikopo ya asilimia 10

Halmashauri ya Jiji la Dodoma Kuhudumia Majimbo Mawili ya Uchaguzi