Halmashauri ya Jiji la Dodoma Kuhudumia Majimbo Mawili ya Uchaguzi
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imejipanga vema kutoa huduma kwa wananchi wote kwa kuzingatia
mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini wenye mapendekezo ya kuligawa jimbo hilo kuwa
Jimbo la Mtumba lenye jumla ya kata 20 na Jimbo la Dodoma Mjini lenye kata 21.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, mara baada ya majadiliano kutoka kwa Madiwani kuhusu taarifa iliyowasilishwa na Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Albert Kasoga ya kuwasilisha mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani lililofanyika tarehe 12 Machi, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Dkt.
Sagamiko alisema “mgawanyo huu kwa sasa unalenga mgawanyo wa jimbo kuwa majimbo
mawili, bado tutaendelea kuwa na halmashauri moja kwa maana ya utoaji huduma kwa
ngazi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Jiji litaendelea kuwajibika katika
utoaji wa huduma katika majimbo yote mawili”.
Akizungumzia
kuhusu mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, alisisitiza kuwa, mgawanyo huo
utazingatia zaidi kata na sio tarafa. “Kwa minajili ya jambo letu la leo la
kupendekeza mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, tutaangalia zaidi kata na wakati
utakapofika kutoa mapendekezo ya mgawanyo wa tarafa na mtaa kwa mamlaka zile
basi tutarejea tena katika utaratibu wa kawaida” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Sambamba na hilo, alitoa rai kuwa, baraza lijikite katika mipaka ambayo inatambulika kwa mujibu wa sheria “nilikuwa nashauri baraza lako lijikite katika mipaka ambayo kwa sasa inatambulika kwa mujibu wa sheria, kwamba tunazo kata 41 na mitaa 222. Hivyo, vingine kwa sasa bado hatuna. Kwahiyo, mipango yetu yote nashauri tuweze kujikita hapo na pale itakapopendeza taratibu nyingine zitaweza kufuatwa” alishauri Dkt. Sagamiko.
Mgawanyo
wa Jimbo la Dodoma Mjini umezingatia hali ya kiuchumi ya jimbo hasa suala la
ukusanyaji mapato, lengo ikiwa ni kuona maeneo yaliyopo juu kiuchumi hayamezi
kiuwakilishi maeneo yaliyo chini kiuchumi.
MWISHO
Comments
Post a Comment