Maafisa Mazingira Kanda Namba Sita waanza ziara ya kutoa elimu ya usafi wa mazingira sambamba na uhamasishaji wananchi kuchangia ada ya uzoaji taka.
Maafisa Mazingira Kanda Namba Sita waanza ziara ya kutoa elimu ya usafi wa mazingira sambamba na uhamasishaji wananchi kuchangia ada ya uzoaji taka.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika baina ya watumishi wa Kanda na viongozi wa Mtaa wa Mbwanga, Afisa Afya Kanda Namba Sita, Zainab Iddi alisema kuwa kuishi kwenye mazingira safi ni haki na wajibu wa kila mwananchi
Alisema kuwa usafi wa mazingira husaidia afya kuwa imara na salama. "Mtaa wa Mbwanga ni mojawapo wa mitaa ambayo tunataka wananchi waimarike katika suala la usafi wa mazingira. Katika suala la kiafya hairuhusiwi kutunza taka kwa mda mrefu au kuzichoma kwasababu kuna baadhi ya kemikali zinaweza kuleta madhara kwa binadamu" alisema Iddi
Aidha aliongeza kuwa wananchi wanatakiwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Akisoma sheria za usafi wa mazingira Afisa Mazingira Kanda, Lillian Itonge alisema kila mwanchi anatakiwa kutoa ada ya uzoaji taka.
"Kuna viwango tofauti vya ada ya uzoaji taka kutokana na mazingira kwa mfano, kaya inatakiwa kulipa shilingi 5,000 kwa mwezi, mwenye mgahawa atalipa 50,000 kwa mwezi na nyumba ya kulala wageni ni 30,000. Fedha zote hizo zinaingia kwenye mapato ya halmashauri ambazo zitawawezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo" alisema Itonge.
Kwa upande wake mdau wa mazingira ambaye anahusika katika uondoshaji wa taka katika Kata ya Mnadani, Mathew Gwau alisema kuwa yupo tayari kushirikiana na uongozi wa Mtaa wa Mbwanga ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama. "Tutapanga ratiba ambayo itakuwa ikionesha siku ambazo tutakuwa tukipita kuchukua taka katika Mtaa wa Mbwanga. Lakini pia tupo katika zoezi la kuwatambua wananchi ili tuweze kuwaweka katika mfumo ambao utatumika kutoa taarifa ya kuwa siku gani gari litakuwa likipita kuchukua taka na pia kuwakumbusha muda wa kulipa ada ya taka" alisema Gwau.
MWISHO
Comments
Post a Comment