TLS yashauriwa kusimamia haki na usawa nchini
Na. Janeth Gerald, DODOMA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.
Dotto Biteko amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na mawakili
kusimamia haki na usawa nchini ili kuhakikisha haki inatendeka kwa watu kwa
lengo la kuchochea maendeleo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko
Kauli hiyo aliitoa wakati akimuwakilisha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa (TLS)
uliofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Biteko alisema, TLS wakati inaadhimisha
miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, wanachama wake wanatakiwa kutafakari mwelekeo
wa chama hicho kitaaluma ili kuendana na azma ya serikali ya awamu ya sita
ambayo imeweka nia thabiti katika kuhakikisha haki inaonekana ikitendeka.
"Tumieni muda kusema na kusikiliza hoja
za watu wanaojua na wasiojua kwa kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria
kuhakikisha kuna hekima mahala pa kazi" alisema Dkt. Biteko.
Aidha, aliwataka wanachama wa TLS kutumia
taaluma yao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini baadae
mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwakani. Aliwahimiza kuchagua
viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo badala ya kuzingatia tofauti nyingne
zinazo watofautisha binadamu.
Akizungumzia uchaguzi ndani ya TLS, Naibu Waziri
Mkuu aliwataka wajumbe kuchaguana kwa kuzingatia vigezo, nia na mwelekeo wa
wagombea watakao kiwezesha chama hicho kusonga mbele na siyo wale
wataotanguliza maslahi binafsi badala ya chama.
Nae, Rais wa TLS, Wakili Harold Sungusia alisema
kuwa katika kitabu cha orodha ya mawakili nchini idadi ya mawakili imefikia 12,471.
Alisema kuwa ongezeko hilo la mawakili litasaidia kutatua changamoto zilizopo
za kisheria.
Akiongelea tabia ya kukamata kamata mawakili
wakati wakitekeleza majukumu yao vimepungua. "Vitendo vya kukamatwa kwa
mawakili hadharani wakati wakiwakilisha wateja wao vimepungua sana
ikilinganishwa na miaka iliyopita. Tunatamani useme neno Mheshimiwa mgeni rasmi
ikiwezekana kwa kuwa ni aibu wakili kushikwa ‘Tanganyika jeki’ akiwa
kazini" alisema Wakili Sungusia.
Habari hii imehaririwa na Frola Nadoo
MWISHO
Comments
Post a Comment