Maandalizi ya Nanenane 2024 Dodoma yapamba moto

Na. Flora Nadoo, DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri ampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka alama katika maboresho ya miundombinu ya maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati Dodoma.



Kauli hiyo aliitoa mjini Dodoma alipokuwa akiongelea maandalizi ya maadhimisho ya sherehe za Nanenane zinazofanyika katika viwanja vya Nanenane Nzuguni.

Alhaj Shekimweri alisema kuwa mwaka jana Rais wakati akiahirisha maonesho ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwenye Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya alielekeza maboresho ya viwanja vya Nanenane.

Alisema kuwa viwanja viwili vimechaguliwa kuanza kufanyiwa ukarabati. Alisema kuwa Waziri wa Kilimo, Husein Bashe na viongozi wa Wizara chini ya Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Gerald Mweli wameanza ukarabati wa viwanja hivyo. “Tumeanza kufanya kazi mbalimbali, miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na udhibiti na uendeshaji wa uwanja kwa kujenga uzio, kujenga sehemu ya upashanaji habari (Information Centre).

Shekimweri alisema kwenye maonesho hayo ya Nanenane kutakuwa na mitambo ya kuchakata kwenye kilimo kama vile trekta, pawatila na nyingine nyingi. Wazalishaji wa vifaa hivyo watakuwepo, kila anayehusika na tasnia ya kilimo atakuwepo ili wananchi aweze kuona, kujifunza, na kuchangamkia fursa zinazotokana na shughuli za maonesho.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alisema kuwa anategemea kuwa na watu wengi sana watakaoshiriki maonesho hayo ikiwemo taasisi za kimataifa pamoja na nchi za jirani zisizopungua tano na taasisi 45 zimethibitisha kushiriki katika maonesho hayo.

Aliongeza kuwa Dodoma ni kanda pekee yenye paredi ya mifugo. kutokana na maonesho hayo masoko ya wakulima yanaweza yakaanza kuunganishwa nje ya nchi na kwa namna hiyo wakulima watapata thamani kubwa sana kutokana na kazi kubwa wanayoifanya na jasho wanalolitumia.

Maadhimisho ya Nanenane mwaka 2024 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’.

 

Habari hii imehaririwa na Emmanuel Lucas akishirikiana na Janeth Gerald

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma