Nanenane ni muhimu kujifunza Kilimo na Ufugaji bora
Na. Rahma Abdallah na Jackline Patrick, NANENANE
Maadhimisho
ya siku ya wakulima Nanenane ni maonesho ya muhimu ambayo humwezesha mwananchi kujifunza
katika kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi. Maonesho hayo ni mahususi kwa kila
mtanzania katika kuzalisha mazao yenye tija kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Hayo
yalizungumzwa na Diwani wa Kata ya Kikombo, Emmanuel Manyono alipokua
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya kimataifa ya Nanenane
jijini Dodoma.
Manyono
alisema kuwa maadhimisho hayo yanaleta tija kwa jamii na pia kuwapa wakulima elimu
ya kilimo na ufugaji bora. “Maonesho haya yamekua yakileta tija, kumekua na
mafunzo mengi yakisaidia wakulima kuondokana na kilimo cha zamani na sasa
kulima kwa kuzingatia kilimo cha kisasa. Kilimo cha kisasa kinamafanikio
makubwa, mkulima analima shamba dogo linalotoa mazao mengi na bora. Hivyo, rai
yangu wakulima wajifunze kulima kilimo cha kisasa. Wananchi wajitokeze katika
maonesho ya Nanenane hapa Nzuguni kujifunza mbinu bora za kilimo cha kisasa na
matumizi ya teknolojia za kilimo’’ alisema Manyono.
Pia
alisema kuwa kuwepo kwa maonesho hayo kunaleta chachu kwa wakulima nchini
kutokana na fursa zinazotolewa kwa wakulima wote katika uuzaji wa mazao kwa
kunufaika zaidi na kilimo chao. Tofauti na mfumo wa kizamani ambao ulikua ukiwanyonya
wakulima, aliongeza.
Akiongelea
changamoto zinazowakabili wakulima, alisema ni uelewa na kufuata maelekezo ya
wataalam kuhusu kilimo bora. “Maonesho ya Nanenane yanasaidia utoaji wa elimu
kwa sababu wananchi wanaelimishwa huku wakiona kwa macho. Hivyo, maonesho haya
yanaleta mabadiliko kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hivyo, nawaomba
wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika mabanda has abanda la Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kwa ajili ya kupata elimu ya kilimo bora’’ alisema Manyono.
Maadhimisho
ya kimataifa ya Nanenane kanda ya Kata yalianza tarehe 1-8 Agosti, 2024
yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa
maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’.
MWISHO
Comments
Post a Comment