Wananchi 2,700 Kunufaika, Mradi wa Ukarabati Maji Taka

Na. Faraja Mbise, KIWANJA CHA NDEGE

Takribani wakazi 2,700 wanatariwa kunufaika na mradi wa ukarabati wa mtandao wa maji taka unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) katika Mtaa wa Area C na D, Kata ya Kiwanja cha Ndege, jijini Dodoma.


Hayo yalisemwa na Mhandisi wa Maji taka DUWASA, Mhandisi Yohana Koroso alipokuwa anawasilisha taarifa ya mradi wa ukarabati wa mtandao wa Maji taka katika eneo la Area C na D wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma.

Mhandisi Koroso alisema “mradi unagharimu jumla ya shilingi bilioni 4.9 ambao utawezesha jumla ya watu 2,700 kunufaika na mradi huo katika uondoaji wa Maji taka”.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, alisema ukarabati wa miundombinu ya Maji taka una urefu wa Kilomita 19 za mabomba ya plastiki (PVC). Mhandisi Koroso alisema “ukarabati wa miundombinu ya maji taka maeneo ya Area C na D wenye urefu wa Kilomita 19 za mabomba ya plastiki (PVC) kuanzia kipenyo cha 160mm hadi 315mm”.

Sambamba na hilo, alisema utekelezaji wa kazi za mradi na hatua zilizofikiwa kwa kiwango cha ukamilifu wa mradi huo ni jumla ya asilimia 96. “Kazi za mradi na hatua zilizofikiwa kwa sasa ni ulazaji wa mabomba mapya ya plastiki daraja B na viungio vyake, yenye kipenyo kuanzia 160mm mpaka 315mm ambao umefikia jumla ya mita 19,159 za mabomba kati ya mita 20,274 zimelazwa na ukamilifu wake ni asilimia 94.5. Ujenzi wa jumla ya chemba 936 kati ya 962 zimejengwa na kazi inaendelea ambapo imekamilika kwa asilimia 97.3” alisema Mhandisi Koroso.

Hata hivyo, alisema kuwa kutokana na changamoto kadha wa kadha hasa kuchelewa kwa malipo ya hati mbalimbali za madai ya Mkandarasi, imepelekea mradi kutokukamiliaka ndani ya muda uliopangwa.

Mradi huo wa Maji taka uliandaliwa na DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, utekelezaji wake unafanywa na Mkandarasi Shanxi Constructions Engineering Corporation and Mineral Company chini ya usimamizi wa DUWASA.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma