Bilioni 9.1 yanufaisha vikundi kwa Mwaka 2020-2023
Na. Faraja Mbise, IPAGALA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilitoa
takribani ya shilingi bilioni 9.1 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu ndani ya kipindi cha Mwaka 2020 hadi 2023.
Hayo yalisemwa na Kaimu Afisa Maendeleo
ya Jamii, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alipofanyiwa mahojiano
na waandishi wa habari, mara baada ya kumalizika kwa ziara ya Kamati ya Siasa
ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma kukagua miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika Jiji la Dodoma.
“Kwa mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuanzia Mwaka 2020 hadi 2023,
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.1 ikiwa na
maana vikundi 767 vimepata mkopo. Vikundi vya akina mama 407, vijana 279 na
watu wenye ulemavu 81 hii ni sawa na watu 4,883 wamenufaika na mkopo wa
asilimia 10” alisema Sebyiga.
Akizungumzia kuhusu faida za mkopo wa asilimia
10, alisema kuwa mkopo huo una faida kubwa sana na unawawezesha kuongeza kipato
chao na kuboresha maisha yao kwa ujumla. “Mikopo ya asilimia 10 kwakweli
imewasaidia watu wengi, mfano kikundi tulichotembelea leo, umeona ufugaji
unaoendelea pale pamoja na wao kuweka nguvu yao na serikali imeweka nguvu pale
kwa kiasi walichopata kimewasaidia sana takribani shilingi milioni 20. Hivyo,
imewasaidia maisha yao na hata kipato chao kinakua” alisema Sebyiga.
Sambamba na hilo alisema kuwa kuna
changamoto katika kufanya marejesho hasa kwa vikundi vya vijana kutokana na
kufanya vitu ambavyo ni tofauti na walivyovikusudia kufanya pindi walipoomba
mkopo huo. “Wenye changamoto kubwa ya kurudisha mikopo ni vijana, kwasababu
wanapochukua hii mikopo muda mwingine wanafanya shughuli ambazo wanakuwa
hawajaandika kwenye andiko lao. Natoa ushauri kwamba, wanapochukua hii mikopo
basi wafanye kile ambacho wamekipanga” alisema Sebyiga.
Pia alitoa rai kwa wananchi wenye
vigezo vya kupata mikopo hiyo kuchangamkia fursa kwasababu mikopo hiyo imeletwa
kwa ajili yao. Sebyiga alisema “tunawahamasisha wananchi waende kwenye kata zao
watume maombi na waombe, hii pesa ipo kwa ajili yao waweze kupata hii mikopo ili
iweze kuwasaidia katika shughuli zao za kimaendeleo”.
MWISHO
Comments
Post a Comment