Dodoma Queens yawakalisha Dodoma Jiji
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya mpira
wa kikapu ya wanawake ya Dodoma Queens imeibuka kidedea kwa kushinda vikapu 44
kwa 33 vya Dodoma jiji katika bonanza la kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake
Duniani Machi 8, mchezo uliopigwa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Dodoma.
Akizungumza baada
ya mchezo huo, nahodha wa timu ya Dodoma Queens Respicia Mkulas alisema “mchezo
ulikuwa mzuri,na tumeweza kupata ushindi
wa tofauti ya seti 10, nitoe rai kwa wanawake wenzangu kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michezo
mbalimbali kwasababu michezo ni afya, michezo ni burudani na pia michezo ni
dawa inakukinga dhidi ya magonjwa”.
Nae, Jeni
Kutawe, Nahodha wa timu ya kikapu ya Dodoma Jiji baada ya mchezo kutamatika akawaita
wanawake kote nchini kushiriki kwenye mazoezi ili kuimarisha afya na kupunguza
uwezekano wa kupata magonjwa.
“Mchezo ulikuwa
mzuri tumefurahi japo tumepoteza, mchezo huu ulikuwa siyo wa kushindana ulikuwa
ni mchezo wa burudani kuhakikisha wote tunafurahi na bonanza linaenda vizuri,
ushauri wangu kwa wanawake wote wajitokeze kufanya mazoezi kwa wingi kwani
mazoezi yanasaidia kulinda afya ya mwili” alisema Kutawa.
Wakati
akifungua Bonanza hilo Mgeni David Msasa, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma akatoa wito kwa wanawake kujitokeza ipasavyo kushiriki kwenye michezo
ili kutengeneza usawa katika michezo na jamii.
“Nitoe shime
kwa wanawake waliofika hapa na ambao hawajafika hapa wajitokeze kwa wingi
kufanya mazoezi kwasababu michezo ni afya lakini pia kupitia michezo
tunatengeneza mawasiliano mazuri baina yetu na wengine, niwapongeze sana wale
ambao mmejitokeza kushiriki bonanza hili ikiwa ni maandalizi kuelekea kilele
cha Siku ya Wanawake Duniani, kwahiyo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na Ofisi
ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma zinawatakia kila la kheri” alisema Msasa.
Siku hii ya
wanawake duniani rasmi ilianzishwa tarehe 8 Machi 1975 baada ya Umoja wa Mataifa
kuridhia siku hii kutumika kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake kwa lengo
la kuongeza chachu katika harakati za mapambano katika usawa kwa mwanamke na
mwanamke katika jamii, maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka huu
kitaifa yatafanyika mkoani Arusha yakiwa na kaulimbiu “Wanawake na wasichana
2025: tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji”.
MWISHO
Comments
Post a Comment