Dodoma Jiji FC, yawapigia hesabu kali Wanangushi
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, hii leo itashuka
dimbani kukipiga na klabu ya Soka ya Coastal Union ikiwa ni muendelezo wa
mbilinge mbilinge za duru ya lala salama ya ligi kuu ya NBC Tanzania Bara,
mchezo utakaochezwa katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma, majira ya saa 3
kamili usiku.
Akizungumza wakati wa mkutano kabla ya mchezo, Kocha
mkuu wa Dodoma Jiji FC, Meck Mexime aliweka wazi ugumu wa mchezo kuzingatia
ligi inaelekea ukingoni. “Ligi inaelekea ukingoni mpaka sasa haijulikani nani
anashuka nani anabaki jambo ambalo linafanya kila mchezo kuwa kama fainali. Kila
timu tunayokutana nayo inakuwa imejiandaa vizuri lakini sisi hilo halitutishi
kwasababu maandalizi yetu ni ya kufanya vizuri kwenye kila mchezo bila kujali
ni nani tunaenda kukutana nae, jambo jingine linalofanya mchezo huu kuwa mgumu
ni timu zote mbili tumetoka kupoteza michezo yetu iliyopita. Kwahiyo, kila timu
inaingia kwenye mchezo huu kutafuta matokeo ili kuweza kutengeneza mazingira
mazuri ya kukaa nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, makosa ya mchezo uliopita
tumeyafanyika kazi kwenye uwanja wa mazoezi kesho tunakuja tukiwa na nguvu mpya
na ari mpya kuhakikisha alama tatu zizabaki nyumbani” alisema Mexime.
Nae, mchezaji wa Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, Abdi
Banda akaelezea hali ya kikosi kuelekea kwenye mchezo wa leo dhidi ya Coastal
Union. “Kama wachezaji tumejiandaa vizuri kwenda kukabiliana na Coastal Union
tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini sisi tumejiandaa kwenda kufanya vizuri ili
tuzidi kupanda kwenda nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa ligi, makosa ya
mchezo uliopita tumeshayafanyia kazi na katika mchezo wa leo tunaamini tutapata
matokeo ya ushindi” alisema Banda.
Kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC Tanzania Bara Dodoma Jiji FC, ipo katika nafasi ya saba ikikusanya alama 26, ikishuka dimbani mara 21, ikishinda michezo saba, ikitoka sare michezo mitano, ikipoteza michezo tisa, ikifunga mabao 22, ikiruhusu wavu wake kutikiswa mara 27.
Habari hii imehaririwa na Nancy Kivuyo
MWISHO
Comments
Post a Comment