DUWASA yamshukuru Rais, Dkt. Samia kutoa kipaumbele huduma za Maji

Na. Faraja Mbise, DODOMA MAKULU

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) yamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele katika kutatua changamoto za upatikanaji wa Maji mjini Dodoma.


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kutoa Maji Njedengwa kupeleka mpaka UDOM, Mhandisi wa Usambazaji Maji, Peter Shemwelekwa kutoka DUWASA, alisema kuwa mamlaka inaendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa Maji katika maeneo mbalimbali mjini Dodoma na pembezoni. “DUWASA ilipewa maelekezo na Wizara ya Maji kuongeza Maji katika busta ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ili kusaidia kuongeza kiwango cha Maji katika matanki yaliyopo (UDOM). Kutokana na Changamoto ya Maji kuwa kubwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma. DUWASA iliamua kutoa Maji kutoka bomba kubwa la inchi sita linalotoka katika Tenki la Njedengwa na kupeleka Maji katika Tenki la kukusanyia Maji kabla ya kusukumwa kwenda maeneo mbalimbali ya UDOM. Mradi huu pia unalo tawi linalohudumia nyumba za NHC Iyumbu, pale itakapolazimu. Mpaka sasa mradi huu umekamilika na tayari umeshaanza kuhudumia Chuo cha UDOM” alisema Mhandishi Shemwelekwa.

Akiongelea hatua ya utekelezaji, alisema kuwa mradi ulianza kutekelezwa tarehe 24, Januari 2024 na kukamilika tarehe 2 Machi, 2024, ukihusisha ulazaji wa mtandao wa mabomba pamoja na viungio vyake wenye urefu wa kilomita 4.564. Mradi huo umepunguza kero ya upatikanaji wa Maji safi na salama katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) baada ya kukamilika kwake, aliongeza.

Mradi wa Maji safi Njedengwa-NHC-UDOM ulitekelezwa kwa fedha za serikali kuu kiasi cha shilingi 291,338,460 umekamilika kwa asilimia 100.

MWISHO


Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma