Wananchi wahamasishwa kujitokeza kuapata huduma Kanda ya Viwandani, Dodoma
Na. Veronica John, DODOMA
Mkuu
wa Kanda ya utoaji huduma ya Viwandani katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Lucas
Nkelege amewataka maafisa waliopangwa katika kanda hiyo kuhamasisha wananchi
wote wanaojitokeza kupata huduma wanapatiwa huduma kwa viwango vya juu ili
waweze kujivunia utendaji kazi wa wafanyakazi hao wa serikali.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akiongea na wafanyakazi waliopangwa katika kanda hiyo na viongozi wa serikali za mitaa katika kuitambulisha kanda ya utoaji huduma ya Viwandani iliyopo katika jengo la Soko la wazi la Machinga, eneo la Bahi road jijini Dodoma.
Alisema
kuwa moja ya jambo muhimu ni kuhakikisha wananchi wa kata zote wanapata huduma
kwa urahisi. “Katika kanda hii ya Viwandani, tuna kata saba ambazo
tutazihudumia. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwasisitiza tu utoaji huduma bora na
za viwango ili wananchi wafurahie utumishi wetu. Huduma zote zitatolewa hapa,
ila nisisitize zaidi eneo la utoaji wa leseni za biashara na ushuru wa huduma.
Nimeamua kutaja huduma hizi mbili ambazo ilikuwa lazima kuzifuata ofisi kuu ya
halmashauri. Kwa mapenzi mema ya serikali kwa wananchi wake ikaona iwasogezee
huduma kwa ukaribu katika maeneo yenu” alisema Nkelege.
Kwa upande wake Afisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Evodius Nkyabonaki alisema kuwa kupitia kikao hicho alitoa elimu ya masuala ya biashara na uendeshaji wake. “Kupitia kikao hiki pia tumepata nafasi ya kutoa mafunzo na elimu kwa maafisa na viongozi wa serikali za mitaa jinsi malipo ya leseni za biashara pamoja na ushuru wa huduma unavyotolewa na gharama ambazo kila aina ya biashara inapaswa kulipiwa. Hivyo, niwasisitize na maafisa wote kwenda katika kata zao na mitaa yao kutoa elimu hii kwa wananchi wote wanaojishughulisha na biashara. Pia, nawakumbusha maafisa watendaji wote wa kata na mitaa wawe wanapita kwenye mitaa yao na kufanya ukaguzi kuhakikisha wafanyabiashara wana leseni za biashara kwa mujibu wa sheria” alisema Nkyabonaki.
Alisema
kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kuwa na vitambulisho ambavyo watavitumia
kufanya maombi ya leseni za biashara. Pia alitoa rai kwa wafanyabiashara wote
katika kanda hiyo kufika katika ofisi ya kanda ya huduma kwa ajili ya kukata
leseni ya biashara.
Kwa
upande wake, Afisa Afya wa Kata ya Kilimani, Loveness Lyimo alisema kuwa kupitia
kikao hicho wamejifunza vitu vingi kutoka kwa afisa biashara na kuwahamasisha
wananchi kujitokeza kupata huduma katika Kanda ya Viwandani. “Kwa kweli
tunaishukuru sana Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kusogeza huduma hizi karibu
zaidi na wananchi kwasababu hapo awali wananchi wakihitaji huduma ilikuwa
lazima waende hadi ofisi kuu ya jiji. Lakini kwa kupitia kanda tunaweza kupata
huduma kwa urahisi tofauti na awali” alisema Lyimo.
Kanda
ya utoaji huduma ya Viwandani inahudumia kata saba ambazo ni Viwandani,
Majengo, Makole, Kilimani, Hazina, Uhuru pamoja na Madukani.
MWISHO
Comments
Post a Comment