Dkt. Mpango atoa pongezi maandalizi ya Nanenane
Na. Tutindaga Nkwindi, DODOMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango atoa pongezi kwa maboresho katika sekta
ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maonesho ya kitaifa ya Nanenane kwa kuongeza
matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Alitoa pongezi hizo wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya 32 ya wakulima Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa hafla
hiyo, Dkt. Mpango alieleza kuwa serikali imefanya maboresho makubwa
yanayoonekana katika sekta hizo, ikiwemo kuimarisha uhifadhi wa mazao ya
wakulima, utoaji wa chanjo kwa mifugo, na utambuzi wa mifugo kwa kutumia
teknolojia ya kisasa.
Aidha, alisisitiza dhamira
ya serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha chakula barani Afrika kwa kuweka
mkazo kwenye uzalishaji wa mazao ya kimkakati yenye thamani kubwa ili kuwavutia
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. “Viongozi wote katika ngazi mbalimbali
wanapaswa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera za kilimo na kuwahimiza
wananchi kutumia ardhi kwa tija, hususani kulima mazao yanayostahimili ukame”
alisisitiza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa maonesho ya
Nanenane ni kiashiria cha uwezo wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuwa na
upatikanaji wa chakula cha kutosha. “Ndugu wananchi, sekta ya kilimo imeendelea
kufanya vizuri sana na inaashiria upatikanaji wa chakula ni toshelevu. Wataalam
waendelee kutusaidia kutoa elimu ya kutosha na kufanya tafiti yakinifu katika
kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi” alisema Dkt. Mpango.
Maonesho ya Nanenane hutoa fursa kwa wakulima, wafugaji, na wavuvi kutoka maeneo mbalimbali nchini kuonesha ubunifu, teknolojia, na mafanikio waliyopata katika sekta zao. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi, 2025.
MWISHO
Imehaririwa
na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment