Kuwahi Kliniki Wajawazito kunaokoa Maisha ya Mama na Mtoto
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Wanawake wametakiwa
kuhudhulia kliniki pale watakapo gundua kuwa ni mjamzito ili kuhakikisha afya
bora ya mama na mtoto tangu hatua za awali za ujauzito na kujua maendeleo ya mtoto
na kuepusha magonjwa mbalimbali.
Hayo aliyasema Afisa Muuguzi Msaidizi wa Kituo cha Afya Ilazo, Anita Rweyemamu wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani, yanayofanyika kuanzia tarehe 1-7 Agosti, 2025.
Alisema kuwa wengi wa wanawake
wanaanza kuhudhuria kliniki wakiwa tayari na mimba za miezi mitatu au zaidi
jambo ambalo ni hatarishi kwa afya ya mama na mtoto. “Niwakumbushe akina mama
kuna magonjwa mengi ambayo ni ya kuambukiza na yasio ambukiza yanaweza
yakakukumba ikiwa ni ugonjwa wa kifafa cha mimba. Hivyo, basi mama mjamzito anatakiwa
aanze kliniki mapema ili aweze kupatiwa huduma muhimu kama chanjo, virutubisho
na ushauri wa kiafya. Lakini pia, tunawahimiza wenza wenu kufuatilia na
kushiriki kliniki, kwani jukumu la malezi na afya ya mtoto ni la pamoja”
alisema Rweyemamu.
Kwa upande
wake mwananchi wa Kata ya Nzuguni, Amina Juma alitoa wito kwa wananchi wenzake
kuhakikisha wanahudhuria kliniki kwa wakati ili kulinda afya zao na watoto wao.
“Tumepata mafunzo mazuri kutoka kwa wauguzi wa Kituo cha Afya Ilazo na nitoe
rai kuwa ni muhimu sana kwa kina mama wajawazito kuhakikisha wanahudhuria
kliniki mara kwa mara. Hii husaidia kugundua changamoto za kiafya mapema na
kupata ushauri sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya” alisema Juma.
Maadhimisho hayo yameambatana na elimu kwa wazazi kuhusu lishe bora, unyonyeshaji na umuhimu wa huduma za afya za mara kwa mara kwa watoto wachanga, chini ya kaulimbiu isemayo “Thamini unyonyeshaji, weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto”.
MWISHO
Comments
Post a Comment