Maziwa ya Mama ni kinga kamili kwa Mtoto
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Wazazi wametakiwa
kuhakikisha wanawanyonyesha watoto wao maziwa ya mama kwa kipindi kinachopaswa
ili kuwajengea afya bora na kusaidia ukuwaji wa akili zao, hasa katika miaka ya
awali.
Wito huo ulitolewa na Afisa Lishe wa Jiji la Dodoma, Alfa Fanuel wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani, yanayofanyika kuanzia tarehe 1-7 Agosti, 2025 uliofanyika katika Kituo cha Afya Ilazo, katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alisema kuwa unyonyeshaji wa
maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ni msingi muhimu wa afya ya
mtoto, na huchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuwaji wa ubongo na kinga dhidi
ya magonjwa mbalimbali. “Utafiti unaonesha kuwa watoto wanaonyonyeshwa ipasavyo
huwa na uwezo mzuri wa kiakili, kuwa na kinga thabiti ya mwili, huwa na nafasi
kubwa ya kuepuka utapiamlo na maradhi ya mara kwa mara” alisema Fanuel.
Aidha, alihimiza jamii
kuondoa mila na desturi zinazokatisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto.
“Wajibu wa baba pamoja na jamii kwa ujumla kuwapa wanawake msaada wa kihisia na
kimazingira ili waweze kunyonyesha kwa ufanisi, na kuepukana na mila potofu
kuhusu kumnyonyesha mtoto” alisema Fanuel.
Kwa upande wake mwananchi wa Kata ya Nzuguni, Amina Juma alitoa wito kwa akina mama kuhakikisha wanawanyonyesha watoto wao kwa kipindi kilichopendekezwa na wataalamu wa afya na kuwapongeza watumishi wa Kituo cha Afya Ilazo kwa kuwapatia elimu hiyo. “Ni wajibu wa kila mama kuhakikisha mtoto ananyonyeshwa kwa miezi sita ya mwanzo bila kupewa chakula kingine chochote. Hii ni kinga ya asili inayosaidia mtoto kuwa mwenye afya bora na akili kwa ujumla na niwapongeze watumishi kwa kutupatia elimu hii na sisi tutakuwa wajumbe wazuri kwa kuwaelimisha akina mama wengine” alisema Juma.
Maadhimisho hayo
yameambatana na elimu kwa wazazi kuhusu lishe bora, unyonyeshaji na umuhimu wa
huduma za afya za mara kwa mara kwa watoto wachanga.
Comments
Post a Comment