DC Dodoma awapongeza wahitimu mafunzo ya stakabadhi
Na. Veronica Elias,
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri amewapongeza
wakufunzi wa semina ya usimamizi wa mafunzo ya stakabadhi kutoka wizarani na
washiriki waliohitimu mafunzo hayo na kusema kuwa ni mafunzo muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari Shekimweri alisema kuwa mafunzo
hayo yanaumuhimu kwa wakulima na wafanyabiashara kwasababu yanawawezesha kuona
faida ya kile wanachokifanya pamoja na kupata mabalozi wengine kwaajili ya
kwenda kutoa elimu kwa wakulima.
Alisema kuwa kutakuwa na mfumo rasmi wa kuratibu tasnia ya
mazao mchanganyiko ilikusudi mkulima alindwe na anufaike na jasho lake kupitia
nguvu na gharama alizopoteza kwenye uwekezaji huo Pamoja na wafanyabiashara kupata
haki yao ya msingi kutokana na matarajio yao waliokusudia. “Najisikia furaha
sana kufika katika semina hii kwasababu moja ya maoni yangu binafsi, mfumo wa
stakabadhi wakati fulani unakutana na wapinzani kwa sababu ni kitu kipya
ambacho hawakijui kwa muda huo. Hivyo, asilimia kubwa ya watu kukataa hayo
mabadiliko ni maumbile ya kibinadamu. Moja ya ufumbuzi wa watu ambao wanapinga
mfumo huu ni kutoa elimu na uhamasishaji wa mfumo wenyewe ambao ni meneja, watu
wa rekodi, wasimamizi na watu wanaotunza kwenye maghala. Hapo wakipata mafunzo
hata wakulima wanaokuja wanaweza kuwaelimisha na wanunuzi pia kwa namna moja
ama nyingine” alisema Alhaj Shekimweri.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Zainabu Shomari alieleza kuhusiana
na jinsi alivyonufaika na mafunzo na vitu vipya ambavyo amejifunza kupitia
fursa hiyo. “Sipo kwenye kampuni ya aina yeyote bali nimekuja kwenye mafunzo
kama mtu binafsi na katika msimu wa mafunzo 2025-2026 kitu kipya ambacho
nimejifunza ni uingizaji wa ‘data’ kieletroniki. Pia na sheria ambazo zimewekwa
zimetiliwa sana mkazo na ndizo zinatumika kurekebisha makosa maana kipindi cha
nyuma watu walikuwa wanafanya makosa kwa makusudi. Wakulima watarajie mambo
mazuri kupitia mazao yao na wakae wakijua yapo salama hata wanapokuwa wanatumia
kuyapeleka ghalani” alisema Shomari.
Comments
Post a Comment