RC Dendego apeleka salamu za Waziri Bashe Nanenane
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego aeleza kuwa
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza vipaumbele vya
kilimo ili kuongeza tija za uzalishaji, kuchangia ongezeko la ajira pamoja na
ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo.
Aliyasema hayo wakati akisoma salamu za Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa ufunguzi wa maonesho Nanenane ya wakulima, wafugaji na wavuvi uliofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma kuanzia tarehe 01 – 08 Agosti, 2025.
Alisema kuwa zipo hatua zitakazosimamiwa na wizara
katika kuhakikisha nchi inakua na chakula cha kutosha wakati wote. “Wizara
inatazamia kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe, kuimarisha upatikanaji
wa masoko, mitaji na mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi. Pia kuimarisha
maendeleo ya ushirika na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika
uendelezaji wa sekta ya kilimo” alisema Dendego.
Alimalizia kwa kusema kuwa wizara imeendelea
kuwashauri, kuwaelimisha na kuwawezesha wakulima kuzingatia sheria na maelekezo
ya wataalam ya kutunza mazingira, kulinda vyanzi vya maji, kupanda miti na
kuzingatia matumizi sahihi ya teknlojia za kilimo.
Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa viongozi wanapaswa kusimamia kikamilifu uwezeshaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kiuchumi. “Wakulima wawezeshwe kupata elimu ya huduma za ugani ikiwemo kukuza matumizi ya kanuni bora za kilimo. Halikadhalika kuhamasisha maendeleo ya ushirika na ushirikiano kati ya wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti, maafisa ugani na watunga sera” alisema Dkt. Mpango.
Makamu wa Rais alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kilimo nchini yanatokana na juhudi mbalimbali za wakulima, wafugaji, wavuvi, wadau wa maendeleo pamoja na jitihada za pekee za serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta hiyo.
MWISHO
Comments
Post a Comment